Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pombe ‘feki’ zafurika, wanywaji hatarini

Pombe kali kwenye glasi

Muktasari:

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali nchini, umebaini kuwa watu hao hununua pombe hizo feki, zinazotengenezwa kienyeji vichochoroni na kuwekwa katika chupa na ‘viroba’ zilizo na nembo za kampuni halisi zi nazozalisha pombe hizo.

MAELFU ya wanywaji wa pombe hasa pombe kali, wako katika hatari kupata magonjwa ya ini na upofu wa macho kutokana na kufurika kwa pombe ‘feki’ katika maeneo mbalimbali nchini ambazo huzinywa.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali nchini, umebaini kuwa watu hao hununua pombe hizo feki, zinazotengenezwa kienyeji vichochoroni na kuwekwa katika chupa na ‘viroba’ zilizo na nembo za kampuni halisi zi nazozalisha pombe hizo.

Pombe hizo feki huuzwa katika hoteli, baa, grosari, vibanda vya pombe za kienyeji na meza za wafanyabiashara ndogondogo zilizogaa maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwamo masoko na vituo vya mabasi.

Uchunguzi huo umebaini kuwepo kwa mtandao wa vigogo, wanaojihusisha kuhujumu viwanda na kampuni zinazotegeneza pombe hizo nchini kwa kutengeneza pombe feki.

Pombe zinazotengenezwa kienyeji na mtandao huo wa wafanyabiashara wakubwa na baadhi ya watu waliokaribu na vigogo wa siasa nchini ni pamoja aina ya Whisky, Vodka, Valuer, Gin, Konyagi na Kiroba Original.

Uchunguzi umebaini kuwa kazi hiyo ya kutengeneza pombe feki inafanyika katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Singida.

Jijini Dar es Salaam kazi hiyo inafanyika katika maeneo ya Manzese, Tandika na Kitunda.

Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam, John Kwilasa mkazi wa Mbezi Beach Mtaa wa Yekeyeke alisema kuwa baadhi ya wanawake huuza konyagi feki hasa za paketi maarufu kama viroba.

“Siku hizi kuna konyagi feki zinauzwa pale mtaani kwetu. Kuna siku nimeagiza nikaletewa kiroba, nilipokunywa nikashangaa kusikia ladha nyingine. Nilipowauliza wenzangu nikaambiwa huwa kuna pombe feki, niwe makini,” alisema Kwilasa.

Mfanyabiashara Chriss Martin anayefanya biashara katika miji ya Mwanza, Moshi na Dar es Salaam, alisema kuwa kuzagaa kwa pombe hizo ni matokeo ya rushwa katika vyombo vya usimamizi wa bidhaa.

“Juzi juzi nilikuwa Dar es Salaam, nikaagiza pombe aina ya gordon’s na nilipoiweka tu mdomoni nikagundua ni feki, maana hata ladha siyo yenyewe. Niliimwaga na hili ni tatizo, liko miji mingi tu nchini,”alisema.

Uchunguzi unaonyesha kuwa pombe kali zinazotengenezwa kienyeji na kujazwa kwenye chupa za vinywaji halisi ni zile ambazo hupendwa na wanywaji nyingi kati ya hizo zikiuzwa kwa bei nafuu.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, biashara hiyo hufanywa na wafa nyabiashara wenye mtandao mpana ndani ya nje ya nchi kukiwa na vijana walioajiriwa maalumu kukusanya chupa za pombe zilizokwishatumika.

“Zamani ukienda shimo la takataka utakuta chupa za whysky zilizotupwa na baadhi yetu tulikuwa tunazitumia kuweka maji ya kunywa, leo mbona hazipo, nani wanazikusanya?,” alihoji mteja mmoja.

Jeshi la polisi lawamani

Gazeti hili limedokezwa kuwa wafanyabiashara wanaouza pombe hizo feki wanajulikana kwa majina na maeneo yalipo maduka yao, lakini mamlaka zinazohusika likiwamo Jeshi la Polisi, zinaonekana kuzibwa midomo.

Chanzo kimoja kimelidokeza gazeti hili kuwa mwaka uliopita, lori lililosheheni pombe feki lilikamatwa eneo la Majengo mjini Moshi, lakini likaachiwa baada ya mwenye mzigo huo kutoa rushwa ya Sh25 milioni kwa watu waliotajwa kuwa ni wa Serikali.

“Hao watu wa Serikali walikuwa na gari dogo, walipolikamata lile gari walitaka wapewe Sh50 milioni, lakini wakashushana hadi Sh25 milioni. Walimalizana pale karibu na eneo la Fire (Zimamoto),” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Chanzo hicho kimesema kuwa wanaohusishwa na hujuma hizo ni pamoja na wafanyakazi wa kiwanda halisi cha pombe hizo, watengenezaji vifungashio pamoja na kurudiwa kwa matumizi ya nembo za Mamlaka ya Mapato (TRA).

Taarifa zaidi zinasema kuwa wafanyabiashara wanaojihusisha na pombe hizo ni matajiri wakubwa, wenye uwezo wa kuhonga hata viongozi wa polisi, kiasi kushindwa kuwakamata.

“Ukweli ni kwamba mapambano ni magumu hasa kwa kuwa polisi ndiyo wanaotuangusha. Ni kama dawa za kulevya tu. Siyo kwamba askari hawatoshi, tatizo lao siyo waaminifu. Kuna kesi nyingi tu, lakini haziendelei, kazi ni ngumu mno,”alibainisha mtoa habari huyo aliyeomba asitajwe jina kwa sababu za kiusalama.

Kamanda Kandihabi

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu lawama hizo dhidi ya Jeshi la Polisi, Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti Bidhaa Bandia, Emmanuel Kandihabi, aligoma kuzungumzia akidai kwamba yuko safarini Dodoma.

“Sasa hivi mimi niko safarini Dodoma, siwezi kuzungumzia hayo mambo. Wewe nenda kawaulize TBS, Tume ya Ushindani na wengineo, ndiyo kazi yao. Mimi nipo safarini, si unajua tulikuwa na semina huku?,” alisema Kandihabi na kukata simu.

Jinsi pombe feki inavyotengenezwa

Uchunguzi umebaini kuwa watengenezaji hao huchanganya Ethanol na Methanol, ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu na malighafi nyingine zikiwamo manukato yenye harufu ya pombe hizo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Konyagi, David Mgwasa alipoulizwa kuhusu uwepo wa pombe feki zenye nembo ya Konyagi na nyinginezo zinazozalishwa na kiwanda hicho, alikanusha akidai kuwa wameshadhibiti tatizo hilo.

“Nakuhakikishia hakuna kitu kama hicho, tumeshaidhibiti hiyo biashara. Hata kama umeona viroba vyenye pombe feki, hiyo ilikuwa ya zamani. Kama una kiroba chenye Konyagi feki, niletee nitakupa hela,” alisema Mgwasa.

Madhara ya pombe feki

Mwanasayansi Mtafiti katika masuala ya afya, Profesa Watoky Nkya anaeleza kuwa athari za pombe hizo feki zimeanza kuonekana kwa baadhi ya wanywaji, ambao wameanza kupoteza nguvu za macho kuona.

Profesa Nkya alisema kuwa viwanda vingi vya mitaani vinavyozalisha pombe hizo feki havina mashine zinazoweza kutenganisha kati ya ethanol na methanol na pombe kuwa na kemikali zote mbili.

“Methanol ni sumu, ina athari kubwa. Sasa katika kutengeneza pombe, mashine hizi za mitaani mara nyingine zina shindwa kutenganisha Ethanol na Methanol,”alisema.

Profesa Nkya alisema watengenezaji wa pombe hizo feki wamekuwa wakizalisha pombe hizo na kuweka rangi ili ifanane na pombe halisi na kwamba wakati mwingine rangi wanazozitumia zina madhara.

“Hizo pombe kali feki zimezagaa kila mahali, mimi sasa hununua pombe kali kwenye maduka makubwa yanayoaminika tu.Nikienda baa nakwenda na chupa yangu,”alibainisha Profesa Nkya.

Baadhi ya wateja wa aina hizo za pombe wamedai kuwa licha ya macho yao kupoteza nguvu za kuona, wamekuwa wakipoteza nguvu za kiume na wakati mwingine kupata mning’inio (hangover) kali.

Mfanyabiashara mashuhuri wa Moshi anayemiliki mtandao wa baa na migahawa, Christopher Shayo, alisema kuwa tatizo la kuzagaa kwa pombe kali feki ni janga la kitaifa na Serikali inapaswa kuamka na kuchukua hatua.

Shayo alisema kwamba siyo rahisi kutofautisha pombe feki na halisi kwa kuitazama kwa macho, lakini mtu hugundua pombe aliyokunywa ni feki, baada ya saa moja kupita tangu alipoinywa pombe hiyo.

Mikakati ya Serikali

Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia Simwanza alikiri kuwa na taarifa za kuwepo kwa pombe feki, hasa aina ya Kiroba Original’.

“Sisi tunazo taarifa za kuwepo kwa pombe feki aina ya Kiroba Original’ kwa sababu mzalishaji ndiyo ameripoti kwetu, lakini bado hatujawakamata wanaotengeneza feki. Tunaomba kama mna taarifa nyingine mtupe kwa sababu bado tunaendelea kufuatilia hao watengenezaji wa mitaani,” anasema.

Nayo Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC), kupitia msemaji wake Frank Mdimi ilisema kuwa wanashughulikia malalamiko kama hayo ikiwa mzalishaji au mlaji atapeleka kwao malalamiko.

“Sisi hatujishughulishi moja kwa moja na ubora wa vinywaji, ila kama wazalishaji au wanywaji wataleta malalamiko kwetu, tutayashughulikia. Kwa sasa inakuwa vigumu kujua kuhusu uwepo wa pombe hizo feki,” alisema Mdimi.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Leandri Kinabo amekiri kukithiri kwa vinywaji visivyo na ubora, hasa pombe kali.

Alisema kuwa TBS imeunda kikosikazi kinachoshirikisha wadau likiwamo Jeshi la Polisi, Tume ya Ushindani na Mamlaka ya Chakula na Dawa.

“Tunazo taarifa ya tatizo hilo, lakini hatufanyi kazi peke yetu. Tunacho kikosikazi kinachohusisha TFDA, FCC na Jeshi la Polisi kila tunapokwenda kwenye ukaguzi wa bidhaa,” alisema Kinabo.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo hivyo kama ilivyo kwenye ulinzi shirikishi.