Saa 78 zinavyoipambanua hatima ya Chadema kisiasa

Wednesday December 02 2020
chadema pic
By Mwandishi Wetu

Kutoka Jumanne (Novemba 24, mwaka huu), Saa 9 alasiri mpaka Ijumaa (Novemba 27, mwaka huu), Saa 3 usiku ni takriban Saa 78. Hizo ndizo zinazoipambanua hatma ya Chadema kisiasa.

Novemba 24, mwaka huu, saa 9 alasiri waliokuwa wanachama 19 wa Chadema, wanawake, waliapishwa kuwa wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakijaza nafasi ambazo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilizitangaza kuwa ni stahili ya chama hicho.

Novemba 27, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa kuwavua nafasi zote za uongozi wote waliokula kiapo kuwa wabunge kwa jina la chama hicho. Haitoshi, Mbowe alisema, Kamati Kuu Chadema iliwavua uanachama wote 19.

Fedha au heshima?

Taswira ya Chadema na uelekeo wake tangu ilipokataa matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2020, inaweza kuamuliwa na moja kati ya mambo mawili; fedha au heshima. Uamuzi wa wanachama 19 kwenda kuapishwa, kisha Kamati Kuu Chadema kuwafukuza uanachama, unajengwa katika maeneo hayo mawili.

Mjadala uliokuwepo baada ya wanachama 19 wa Chadema kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum ni kwamba chama hicho kilinywea. Kwamba walisalimu amri na kukubali viti hivyo kwa sababu ya fedha. Kuna waliosema kuwa “hakuna mkate mgumu mbele ya chai.”

Advertisement

Baada ya Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kusema chama chake hakikuwasilisha NEC majina ya wabunge viti maalum, mjadala ukabadilika. Kwamba wanachama 19 walioapa kuwa wabunge walifanya hivyo kwa ushawishi wa fedha.

Hata baada ya Mbowe kutangaza uamuzi wa Kamati Kuu, hoja ambayo iliendelea kutawala ni ileile kuwa wanachama hao 19 waliokula kiapo waliamua kusaliti chama chao kwa sababu ya kufuata masilahi ya ubunge.

Oktoba 31, mwaka huu, Mbowe akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu, kwa pamoja na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, walifanya mkutano wa kutotambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Pamoja na tangazo la kugomea matokeo, viongozi hao walitangaza azimio la kufanya maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima mpaka uchaguzi mwingine ungeitishwa chini ya tume huru na haki. Hivyo, walitaka tume za sasa, NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zifutwe.

Kutokana na msimamo huo wa Chadema na ACT, ni wazi aina yoyote ya kukubali sehemu ndogo ya ushindi kwenye uchaguzi huo, ingekuwa ni kwenda kinyume na kile walichoazimia. Unasema uchaguzi haukuwa huru na haki, kisha unakataa matokeo, lakini unakubali nafasi 19 za viti maalumu.

Ndio maana watu waliibeza Chadema kuwa “hakuna mkate mgumu mbele ya chai,” pale walipokwenda kuapa.

Kukaa kwenye mstari sahihi ni kuwa Chadema waliutangazia umma wa Watanzania na walitaka jumuiya za kimataifa kutambua kuwa uchaguzi haukuwa huru na matokeo hayakubaliki.

Hivyo, ili kubaki kwenye madai yao wanapaswa kugomea hata matunda ya upande wao.

Chadema wanapaswa kusimama kwa vitendo na kukataa viti maalum ili kuthibitisha kuwa si kwamba wanalalamikia yale waliyokosa, bali pia hata nafasi walizozipata nazo hawazipokei kwa kuwa si stahili kwao. Huko ndiko kusimamia msingi wa madai bila kuyumba.

Kwa muktadha huo, kitendo cha waliokuwa wanachama 19 wa Chadema kwenda kula kiapo, kilikuwa na athari mbili kwa pamoja. Mosi ni kwenda kinyume na msimamo wa chama. Pili ni kukivua nguo chama kwa umma na jumuiya za kimataifa.

Usahihi wa uamuzi

Mvutano wa viti maalum haukuibuka ghafla, ulianza na kuchukua nafasi. Mkurugenzi wa NEC, Dk Charles Mahera na Mnyika, mara kwa mara walibadilishana maneno kuhusu majina ya wabunge wa viti maalumu kupitia Chadema. Mnyika alisema hawajapeleka majina, Mahera akasisitiza tayari walishapokea majina kutoka Chadema.

Mitandaoni yakaibuliwa maneno kuwa kulikuwa na wanachama wa Chadema waliokuwa wameasi msimamo wa chama, hivyo kupeleka majina ya wabunge wa viti maalumu. Orodha iliyowekwa ilikanushwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee.

Halima alisema majina hayo yaliyokuwa yanasambazwa mitandaoni ni bandia kwa kuwa Mnyika alishasema hakuna jina lililopelekwa NEC.

Kwa mantiki hiyo, angalau tunaweza kubaki kwenye hoja mahsusi kuwa mvutano wa viti maalumu na uteuzi wake kutokea Chadema, ulikuwa unajulikana kwa kila mtu.

Kwa muhtasari huo, maana yake ni kuwa waliokuwa wanachama 19 wa Chadema waliokula kiapo, walikuwa wanajua kila kitu kilichokuwa kinaendelea kuhusu mvutano kati ya kilichokuwa chama chao na NEC, vilevile yote yaliyokuwa yakizungumzwa.

Ukishaupitia muhtasari huo vizuri, ni rahisi kupata jibu kuwa waliokuwa wanachama 19 wa Chadema, hawakufanya kosa la bahati mbaya kuapa, kusema hawakuwa wakijua kama kuapa ingekuwa ni kosa. Walifanya kila kitu kwa kuongozwa na dhamira.

Ipo hoja kuwa wamefukuzwa bila kusikilizwa. Hata Mbowe wakati anatangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema wanawake hao 19 waliandika barua kuomba udhuru wa kutohudhuria mkutano maalum wa kuwahoji kuhusu uamuzi wao kwa sababu ya kuhofia usalama wao.

Kwa kuzingatia mfumo wa utendaji haki asilia, haikubaliki kumhukumu mtu bila kumsikiliza. Unapaswa kusikiliza ukweli wa pande zote zenye msuguano kabla ya kufanya uamuzi. Halima na wenzake 18, hawakusikilizwa. Hilo halina ubishi.

Yupo mtu anaweza kuhoji kuhusu u - haraka wa Kamati Kuu ya Chadema kufanya uamuzi badala ya kungoja siku nzuri zaidi ili watuhumiwa wahojiwe na kujieleza. Ukitazama hoja za Kamati Kuu Chadema, utagundua kuwa wao walisimamia mantiki kuwa waliwapa nafasi Halima na wenzake lakini walishindwa kuitumia.

Hukumu ya Kamati Kuu Chadema imekuwa na matawi mawili; kwanza Halima na wenzake 18 walikaidi msimamo wa chama, wakasaliti, vilevile wakakihujumu. Pili, walikaidi wito wa Kamati Kuu. Kwa jumla, chama chao kilifanyiwa dharau.

Ikumbukwe pia kuwa Kamati Kuu Chadema ilikwenda kufanya uamuzi kipindi cha presha kubwa. Sehemu kubwa ya watu waliojipambanua kuwa wana-Chadema, hususan watumia mitandao, walijenga shinikizo kubwa kwamba Halima na wenzake watimuliwe, vinginevyo hadhi ya chama ingepotea.

Kuna Mwana - Chadema mwingine nje ya Kamati Kuu ya chama hicho anaweza kuwa anajiuliza: “Unasubiri nini kumhukumu mtu ambaye amekwenda nje ya msimamo wa chama waziwazi?” Suala la Halima na wenzake 18 si la chumbani. Lilikuwa hadharani.

Kuna suala la kughushi nyaraka za chama. Kwamba ilikuwaje Halima na wenzake 18 majina yao yapelekwe NEC wakati mamlaka za chama hazikuyapitisha? Pengine ukawepo utetezi kuwa Halima na wenzake hawakuhusika na upelekaji wa majina, bali wao waliitwa tu kwenda kuapa.

Kama ndivyo, ni kwa nini Halima na wenzake 18 hawakutoa taarifa kwa viongozi wa chama kuhusu wito wa kwenda kuapa kabla ya siku ya tendo lenyewe? Hakosekani wa kusema, viongozi wa Chadema waliarifiwa ila waliwageuka. Swali linarudi; Kwa nini hawakuitikia wito wa Kamati Kuu?

Sijasahau kuwa Halima na wenzake walitoa udhuru. Sawa, lakini walijua kuwa Kamati Kuu ya Chadema ilikuwa inakwenda kuketi kwa ajili yao tu. Kwa nini hawakuandika maelezo ya utetezi kuhusu uamuzi wao kwenda kuapa? Pengine kuna hoja wangetoa na zingeeleweka na uamuzi wa Kamati Kuu, ingewezekana kuwa wa tofauti.

Hivyo, kutoka Jumanne (Novemba 24), saa 9 alasiri, siku na muda ambao Halima na wenzake 18 waliapa kuwa wabunge wa viti maalumu kwenye Bunge la 12 kupitia Chadema, hadi Ijumaa (Julai 27), saa 3 usiku, Mbowe alipotangaza uamuzi wa Kamati Kuu, zilikuwa Saa 78 za Chadema kupigania na kupambanua hatma yake ya kisiasa. Fedha au heshima? Inaogopa watu au inasimamia misingi? Chenyewe ni taasisi au kinategemea majina?

Advertisement