Sababu za wazazi kupeleka watoto wadogo shule za bweni

Dodoma. Imeelezwa kuwa kuvunjika kwa ndoa ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanafunzi chini ya darasa la tano kupelekwa shule za bweni.

Hilo limekuja siku chache baada ya Kamishna wa Elimu nchini, Dk Lyabwene Mtahabwa kutoa waraka namba mbili wa mwaka 2023 kuhusu utoaji wa huduma ya kulaza wanafunzi unaozuia wanafunzi chini ya darasa la tano kukaa bweni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi kuhusu suala hilo, baadhi ya wazazi walizitaja sababu za kupeleka watoto wenye umri mdogo katika shule za bweni kuwa ni pamoja na kukosa muda wa kukaa nyumbani, ulezi wa mzazi mmoja, changamoto za wafanyakazi wa ndani na mateso ya watoto.

Beatrice Msigwa alisema kuwa mazingira ya shughuli zinazomletea kipato ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mzazi kumpeleka mtoto katika shule za bweni.

“Unakuta mama ndio baba, atakaaje nyumbani kulea watoto, inambidi kwenda kutafuta fedha ambazo pamoja na matumizi mengine atazitumia kumpeleka mtoto shule na kuihudumia familia yake, hapo analazimika kumpeleka mtoto shule ya bweni. “Halafu kuna wanandoa ambao mmoja wao amezaa nje ya ndoa, anaona mtoto wake anateswa kwenye familia anaamua kumpeleka shule za bweni, ili kumwezesha kuwa na mazingira mazuri kwa malezi na usomaji,” alisema Beatrice.

Kwa upande wa Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu alisema kauli hiyo imetolewa na watu ambao hawajafanya utafiti wa kina kuhusiana na changamoto ya ukatili na unyanyasaji.

Alisema tafiti zinaonyesha watoto wengi wanafanyiwa ukatili nyumbani kuliko shuleni, na mara nyingi wanaogundua watoto wamefanyiwa ukatili ni walimu, kwa hiyo mazingira salama ni shuleni.

Alisema watoto wanapokuwa katika shule za bweni hupangiwa hata utaratibu wa shughuli wanazotakiwa kufanya kwa siku, na kuhoji ni wazazi wangapi wanaweza kuwapangia utaratibu watoto wao wakiwa nyumbani.

Naye Dorothy Mwakipesile alisema alilazimika kumpeleka mtoto wake shule ya bweni baada ya changamoto ya kumpata mfanyakazi wa ndani wa kumlea.

“Mimi niko pekee yangu na mwanangu, kila msichana wa kazi niliyekuwa nampata alikuwa ana changamoto zake ambazo zilinifanya kushindwa kumuamini kumwachia mtoto. Sina pa kumpeleka, baba na mama walishafariki dunia.

Mtoto akawa akitoka shule anafikia kwa majirani hadi ninaporudi kazini,” alisema.

Akilizungumzia hilo, Rebecca Francis ambaye ni mzazi na mkazi wa Tabata, alisema wakati mwingine mazingira yanayozunguka eneo analoishi mtoto ndiyo yanafanya bweni kuonekana kama sehemu salama kwa ajili ya makuzi yake. “Hii sehemu niliyojenga sikujua kama baadaye itazungukwa na baa zinazokesha zikipiga muziki, watu wanakunywa hadi asubuhi wakiwa wamevaa nusu utupu, bahati mbaya sana na biashara ya wanawake kuuza miili yao imeanza kuibuka, siwezi kumuacha mtoto mazingira haya,” alisema Rebecca.

Maneno yake yanaungwa mkono na Faraja Kristomas kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyesema uzuiaji wa huduma za bweni kwa wanafunzi wadogo unapaswa kuangaliwa kwa pande zote, kwa sababu kuna mazingira wakati mwingine bweni ni bora kuliko mtoto kukaa nyumbani.

“Na hili hasa kwa familia zilizotengana, unakuta baba ni mfanyakazi yuko bize muda wote anasafiri, mtoto anabaki nyumbani na ndugu ambao hawana upendo kwa watoto, wanapitia ukatili wa kila aina hivyo ili kumnusuru ni bora akae bweni.


Kuhusu wanaokaa nyumbani

Wakati kukaa nyumbani kwa watoto hawa ikiwa ni kitu kinachozungumziwa kuwa ni salama, Faraja alisema watoto kusafiri umbali mrefu kufuata shule pia huwaweka katika mazingira hatarishi.

Naye Daud Maganga ambaye ni mzazi, alisema watoto wanaotokea nyumbani kwenda shuleni wakati mwingine huwa katika hatari zaidi ya wanaokaa bwenini.

“Mji kama huu (Dar es Salaam) kuna baadhi ya wazazi wana aina ya shule wanazozipenda, tukiacha zile za kulipia hata hizi za Serikali, wewe hujawahi kusikia mtoto anakaa Mbande (Mbagala), anasoma Shule ya Msingi Bunge (Posta), jiulize anaamka saa ngapi anapitia vikwazo gani huko njiani,” alisema.


Nini kifanyike

Licha ya kupongeza uamuzi uliochukuliwa na Serikali, Dk Zubeda Mussa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema umefika wakati wa wazazi kuhakikisha jukumu la malezi wanalitekeleza vyema ili watoto wawe salama.

“Wazazi warudie jukumu lao la msingi la malezi, wana jukumu la kuangalia zaidi mazingira anayoishi mtoto kuyachunguza na kuyafuatilia kwa sababu ukatili unafanywa na wale watu wanaotuzunguza zaidi, ikiwemo ndugu,” alisema Dk Zubeda.