Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Shirikianeni, shikamaneni kupunguza rushwa Afrika’

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleman Abdulla.

Muktasari:

  • Maadhimisho ya siku ya kupambana na rushwa barani Afrika yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kusainiwa mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa yamefunguliwa leo Jumapili, Julai 9, 2023 na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleman Abdulla.

Arusha. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleman Abdulla amezitaka nchi mbalimbali barani Afrika kushirikiana na kushikamana ili kupunguza vitendo vya rushwa barani Afrika.

Abdulla ameyasema hayo leo Jumapili, Julai 9, 2023 jijini Arusha kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati akifungua maadhimisho ya  siku ya kupambana na rushwa barani Afrika.

Pia, yanakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kusainiwa mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa.

Amesema nchi za Afrika zinapaswa kuungana kupambana na rushwa kwani rushwa ni adui na inaathari katika utawala bora na kukuza uchumi.

"Vita dhidi ya rushwa ni yetu sote hivyo lazima tushirikiane na tusiachie taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa pekee kwani swala hili ni la kwetu sote kila mmoja kwa wakati wake," amesema.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti  ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema Tanzania wapo tayari kushirikia kwa vitendo kupitia mkataba huo waliosaini na nchi mbalimbali katika kuhakikisha suala la mapambano dhidi ya rushwa linatokomezwa.

Amesema kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni "kuendeleza uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa Barani Afrika."

Simbachawene kupitia kongamano hilo litakalofanyika Julai 10, 2023 litatoa fursa kwa nchi mbalimbali kupeana na kubadilishana uzoefu namna ya kupambana na rushwa katika bara letu la Afrika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni amesema katika kuadhimisha siku ya kupambana na rushwa barani  Afrika ambayo kilele  kinatarajiwa  kufanyika  Julai 11, 2023 itakwenda sambamba na kongamano  litakalofanyika  Julai 10 jijini Arusha ambalo litawashirikisha wadau mbalimbali.

Hamduni amesema kongamano hilo litahudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo wataweza kujadili masuala mbalimbali ikiwemo uzoefu wa taasisi hizo za kupambana na rushwa barani Afrika.

Amesema wataweza pia kujadili kuhusu mchango wa vijana katika mapambano dhidi ya rushwa pamoja na athari za rushwa katika sekta ya elimu.