TEC yataka Kinga kwa viongozi wote ifutwe
Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeshauri kuondolewa kinga ya kushtakiwa kwa viongozi wa Serikali ili kutoa haki sawa kwa Watanzania wote chini ya Katiba na matakwa ya Mwenyezi Mungu ili waweze kushtakiwa wanapokosea.
Baraza hilo limesema Ibara ya 12 (1) ya Katiba inasema binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, huku kifungu cha 13(1) kinafafanua kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
Hata hivyo, Ibara ya 46 (2) kinasema haitaruhusiwa kufungua shauri dhidi ya Rais na kutoa masharti kadhaa.
Baraza hilo la maaskofu ni miongoni mwa taasisi za dini zilizotoa mapendekezo yake kwa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Mfumo wa Haki Jinai jana jijini Dar es Salaam.
Taasisi nyingine zilizotoa mapendekezo kwenye maeneo tofauti ni; Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).
Mara baada ya kutoka kuwasilisha mapendekezo, Dk Camilius Kassala, mkurugenzi wa hadhi ya utu wa binadamu, idara ya haki, amani na uadilifu wa TEC alizungumza na waandishi wa habari akifafanua suala la kinga kwa viongozi, likiwa miongoni mwa hoja nne walizoziwasilisha.
“Ndiyo maana kuna vuguvugu la Katiba Mpya ili hiyo kinga iondolewe, watu wanaelewa sasa binadamu wote tuko sawa, uwe Rais, bosi, tajiri au kamanda wa polisi wote tuko sawa,” alisema Dk Kassala.
Jambo jingine ni kuhusu mageuzi ya mfumo wa kisheria yaliyotokana na utawala wa kikoloni, uzito wa makosa uendane na adhabu za mahakama, ikiwamo utozaji wa faini ndogo katika ngazi za mahakama za chini ili kupunguza mianya ya rushwa kwa wananchi.
Vilevile, maaskofu hao walishauri kuimarisha mfumo utakaowaweka huru wanataaluma katika utekelezaji wa majukumu yao au wakati wa kuwajibishana bila kuingiliwa na mkono wa Serikali.
“Kwa kuwa Serikali inaundwa na wanasiasa, wanasiasa wana masilahi yao kwa sababu wanataka washinde uchaguzi unaofuata. Kwa hiyo watawatumia wanataaluma kwa masilahi yao kisiasa ili washinde chaguzi zijazo, matokeo yake taaluma zinatumikia siasa, badala ya siasa kutumikia taaluma,” alisema Dk Kassala.
Alisema haki ni msingi wa hadhi ya utu wa kila mwanadamu, hivyo mfumo wa haki jinai unatakiwa kuimarika kwa kuwa kukiuka msingi huo ni chukizo mbele za Mungu.
Hoja hiyo ya TEC kuhusu kuondolewa kinga imeungwa mkono na baadhi ya mawakili waliozungumza na gazeti hili, akiwemo, rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk Rugelemeza Nshala aliyesema, “mimi ni muumini wa usawa na watu wote wanapaswa kuwa na haki sawa kisheria.”
Vivyo hivyo, Wakili Patience Mlowe alisema ni Afrika pekee ndiko viongozi hutukuzwa mithili ya miungu watu, lakini mambo yapo tofauti kwingineko.
Alisema katika mataifa mengine nje ya Afrika viongozi huchukuliwa hatua kila wanapokosea, akitolea mfano Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson aliyeshtakiwa kwa kukiuka sheria wakati wa Uviko-19.
“Hiyo demokrasia tunayoiimba asili yake ni mataifa yaliyoendelea, sasa sisi tunatekeleza demokrasia gani kama tunawafanya viongozi kuwa miungu watu,” alihoji.
Kwa mujibu wa Mlowe, ili kuwa na kiongozi mwadilifu lazima kuwepo na mazingira yanayomjengea hofu ya kutenda kosa akijua kuna hatua atakazochukuliwa.
“Anakwenda kujilimbikizia mali si kutumikia watu, wakiondolewa kinga watakuwa na hofu maana watajua wakitenda kosa watachukuliwa hatua,” alisema.
Mwingine aliyeunga mkono ni mwanasheria nguli na rais wa zamani TLS, Fatma Karume aliyesema kwa kuwa hakuna mwananchi aliye juu ya sheria, hata Rais anapaswa kuondolewa kinga ili kuwe na usawa.
“Rais ni mwananchi kama wengine, hawezi kuwa juu ya sheria, anapokosea anapaswa kuwa chini ya sheria na achukuliwe hatua kama wengine,” alisema.
Akifafanua hilo, Wakili Fulgence Massawe alisema kabla ya marekebisho ya sheria, Rais alikuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya jinai na kwamba mabadililo hayo yaliondoa dhana ya uwajibikaji kwa viongozi hao.
Sheria inayowalinda
Kwa sasa viongozi wakuu wa nchi wa mihimili yote wana kinga ya kutokushtakiwa na badala yake mashauri yote dhidi yao yanafunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo, kinga hiyo inahusu mashauri ya madai tu.
Masharti hayo ya kinga hiyo kwa viongozi yamewekwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 ya mwaka 2020 yaliyojumuisha sheria 13 zilizopitishwa na Bunge Juni 2020.
Sheria hiyo ilifanya marekebisho katika vifungu vya sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi Sura ya 3, inayotaka mashauri yote ya madai dhidi ya viongozi wakuu wa nchi, yafunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Marekebisho mengine yalifanyika katika Sheria ya Masuala ya Rais Sura ya 9, katika kifungu cha 6 ambapo mashauri dhidi ya Rais kwa mambo anayodaiwa kuyatenda yeye binafsi kama raia yaliyoruhusiwa kufunguliwa dhidi yake kwa mujibu wa Ibara ya 46 (2) ya Katiba.
Marekebisho hayo yaliweka sharti mashauri hayo yafunguliwe baada ya Rais kutoka madarakani.
Pia kifungu cha 7 kinaelekeza mashauri yoyote dhidi ya Rais kufunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake.
Katika Sheria ya Maboresho ya Sheria kuhusu ajali mbaya na masharti nengineyo Sura ya 310, kiliongezwa kifungu kipya cha 18 kinachoelekeza kuwa mashauri yanayofunguliwa au maombi yanayoletwa chini ya sheria hiyo dhidi ya uamuzi wa Viongozi wa Kitaifa (Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu) kufunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Bakwata yakosoa Sheria ya Ugaidi
Katika maoni yake kwa Tume hiyo, Bakwata imeshauri kuboresha vipengele vya sheria tano, ikiwamo ile ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002 inayotoa mamlaka kwa polisi kupiga risasi na kumuua mtuhumiwa wa ugaidi kabla ya kuthibitishwa mbele ya mahakama.
“Watuhumiwa wanauawa kabla ya mahakama kuthibitisha, unamuuaje wakati mahakama haijathibitisha? Kwa nini asitumie mbinu nyingine za kumkamata? Kama mahakama ndiyo eneo la kutoa haki, mamlaka haya yanakuwepo kisheria kwa nini?” alihoji mwanasheria wa baraza hilo, Hassan Fatiu.
Mjadala kuhusu suala kama hilo uliibuka baada ya Jeshi la Polisi kueleza umma kwamba uchunguzi wake ulibaini mtuhumiwa wa ugaidi, Hamza Mohammed (30) alikuwa gaidi.
Hamza aliuawa Agosti 25 mwaka huu nje ya geti la Ubalozi wa Ufaransa katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, baada kufanya shambulio na kuua askari wanne, akiwamo mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi na kujeruhi wengine sita.
Fatiu alisema sheria hiyo pia imejenga mtazamo hasi kwenye jamii kutokana na waathirika wengi kuwa kundi la imani fulani.
Maoni hayo yamekuja wakati kukiwa na malalamiko ya baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi, wakiwemo masheikh kusota miaka mingi gerezani bila kesi zao kumalizika.
Sheria ya ndoa
Baraza hilo pia limependekeza kutoifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 au miaka 14 kwa kibali cha wazazi.
Mtazamo huo unakinzana na maoni ya wanaharakati wa haki za watoto na wanawake ambao wamekuwa wakipinga utekelezaji wa sheria hiyo kuwa inakinzana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayomtambua mtoto hadi umri wa 18.
Julai 8, 2016 Mahakama Kuu ilitoa hukumu ikikubali kwamba vifungu hivi vya sheria ya ndoa vinapingana na Katiba kwa kuweka umri tofauti wa kuoa/kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.
Hukumu hiyo ilitolewa kufuatia kesi iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi aliyekuwa akipinga kifungu cha 13 na 17 vya sheria ya ndoa kinachoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa kibali cha mahakama, na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.
Kwa mujibu wa Bakwata, mtoto mwenye umri wa miaka 11, 12 au 13 aliyeingia kwenye kipindi cha balehe aruhusiwe kuolewa kwa uhalali wa mahakama utakaozingatia vielelezo vya kimazingira.
“Mtoto wa kike ana miaka 11, 12 hajaendelea na elimu, kwa nini asiolewe? Ukimuacha huyu ni matokeo ya kupata mimba mtaani.
“Simaanishi kila mtoto wa umri huo aruhusiwe kuolewa ila mahakama itajiridhisha afya yake, mazingira na mengineyo,” alisema mwanasheria wa baraza hilo, Hassan Fatiu.
Uhuru wa mahakama
Ilipofika zamu ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), yenyewe ilishauri maeneo manne yanayohusisha mfumo wa huduma za magereza, utendaji wa Jeshi la Polisi na mhimili wa mahakama chini ya msingi wa biblia, kitabu cha Isaya sura ya 32:17-18 kinachoelekeza habari ya kutenda haki ili amani na utulivu vitawale katika jamii.
CCT inayounganisha makanisa 12 na taasisi 14 zinazoendesha huduma mbalimbali za kiroho, ilishauri kuweka misingi itakayoweka huru mhimili wa mahakama.
Askofu Nelson Makori, mwenyekiti wa Kamati ya Sera, Fedha na Programu wa CCT alisema, “tunataka tuone mahakama ikiwa huru kwa asilimia 100 bila kuingiliwa na chombo chochote, itoe haki bila kupendelea, sawa na sheria za nchi.
“Kwa hiyo kuna mapendekezo kuhakikisha mahakama haiingiliwi na chombo chochote, mtu yeyote,” alisema.
“Pili, mahabusu walindwe, hawajahukumiwa. Sasa wanataabika, wanarundikana huko, maisha ya kibinadamu hayapo na inadhalilisha utu wao, kwa hiyo tumeshauri kushughulikia hilo,” alisema Askofu Makori.
Mengine yaliyomo kwenye mapendekezo yao ni pamoja na kuboreshwa kwa mfumo wa mafunzo utakaosaidia mfungwa kurekebishika tabia na kuweka misingi itakayowezesha Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yao kisheria badala ya kusikiliza maelekezo ya watu wengine.
CPCT na maeneo 30
Mwanasheria na mjumbe wa Kamati ya CPCT, Justine Kaleb alisema wameshauri maeneo takribani 30, ikiwamo hoja ya kufuta adhabu ya kifo inayotajwa kifungu cha 196, chini ya Sheria ya Kanuni ya adhabu sura namba 16.
Alisema baraza hilo limeshauri kufutwa adhabu hiyo na kuweka mbadala wa adhabu ya kifungo cha maisha jela kutokana na sababu kuu nne, ikiwamo ongezeko bila utekelezaji wa adhabu hiyo pamoja na kuingilia kazi ya Mungu mwenye haki hiyo pekee.