TUONGEE KIUME: Sababu tatu kwa nini mzee, mtu mzima hatakiwi kuoa binti mbichi

Sunday September 12 2021
kuoa pc
By Kelvin Kagambo

Tukisema binti mbichi tunamaanisha mtoto mdogo, msichana ambaye umri wake unafanana na watoto wako wa kuwazaa, kama huna watoto basi tofauti ya umri kati yenu wawili ni kubwa kiasi kwamba mnaweza kuwa baba na mwana kabisa. Na leo tunaambiana sababu tatu za kwa nini mzee, mtu mzima unatakiwa uoe mwanamke wa aina hiyo.

Wanasema umri ni namba tu, lakini kama unataka kula pensheni yako gerezani tafuta binti mdogo mwenye miaka 20 oa. Kwa nini? Kwa sababu asilimia kubwa ya ndoa za namna hiyo huwa ni za kupangwa, siyo kwa ajili ya mapenzi, mtoto wa miaka 20 akupende wewe kwa lipi?

Ukifanikiwa kuoa mtoto mdogo namna hii tarajia ndoa isiyokuwa na uaminifu hata kwa asilimia 20, labda umfungie nyororo pembeni ya kitanda asitoke ndani kwako, ukioa ndoa ya namna hii tarajia migogoro kila kukicha, ugomvi kati yako na vijana wadogo wa umri wake wanaommendea kwa sababu ndiyo watu rahisi zaidi yeye kuvutiwa nao. Akiwa karibu nao wana mengi ya kuongea kuliko akiwa na wewe, hii wala haihitaji sayansi kuielewa, wewe ni wa kizamani, yeye ni wa kisasa. Na matokeo yake ni nini? Leo utamkuta kasimama kichochoroni na vijana wenzake wanaokusalimiaga shikamoo, kesho atakurudia nyumbani usiku bila sababu, kesho kutwa utamkuta ndani kwako na vijana hao hao. Utaua, Serikali ya mama Samia itakushughulikia.

Pia oa mtoto mdogo kama unataka kifo chako kisababishwe na mtu mwingine. Dini zinatuambia kila mtu ataonja umauti, sayansi inatuambia hivyo pia na kuongeza kuwa watu waliokula chumvi zaidi wana uwezekano mkubwa wa kutangulia kwa vifo vya asili kama vile magonjwa. Lakini kama unaona mtindo huo unakuchelewesha oa mtoto mdogo ili akupe msongo wa mawazo, presha ipande ichanganyike na sukari utangulie kabla ya siku zako.

Na tatu oa mtoto mdogo kama umechoka kuishi kwenye familia yenye amani. Kuna wazee wanaishi vizuri na familia zao, lakini siku wanaamka tu na kuhisi wanahitaji mke mwingine, tena binti mdogo. Na kwa sababu familia nyingi za Kiafrika wanaume tukiamua jambo hakuna wa kutuzuia, basi wanafanikiwa kuoa.

Sasa mke akishangia ndani ya nyumba familia inatibuka, mifano lukuki tunayo kwenye maisha yetu. Kwa hiyo kama umechoka kuishi maisha ya amani na familia yako, ingiza mke mdogo mdogo.

Advertisement

Lakini nisichoelewa zaidi ni sisi wanaume tuna shida gani? Tufanye una miaka 50 au unakaribia umri huo, halafu unakwenda kuoa mtoto mdogo, unakuwa unataka kugundua nini ambacho hukukiona kwenye miaka 50 ya maisha yako?

Advertisement