‘Wadau washirikishwe changamoto kukatika umeme’

Wadau wa nishati wakifuatilia mkutano
Muktasari:
- Wakati Tanzania ikiwa na rasilimali za kuzalisha umeme wa kutosha, changamoto zikiwamo za usambazaji zimekwaza uzalishaji, hali inayorudisha nyuma uchumi wa nchi.
Dar es Salaam. Kuhusisha wadau muhimu katika uzalishaji wa nishati safi kumetajwa kuwa suluhisho muhimu kwa changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara, ambazo zinaathiri uzalishaji wa viwandani na ujasiriamali, hivyo kukwamisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Tanzania inazo rasilimali kubwa za nishati, ikiwemo gesi asilia inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57.54, ambapo trilioni 47.4 zimegunduliwa katika maeneo ya kina kirefu cha bahari na trilioni 10.12 ziko nchi kavu.
Akizungumza Januari 24 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wadau wa nishati na wakurugenzi wa viwanda, Naibu Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Tarak Jani, amesisitiza madhara ya kukatika kwa umeme kwa viwanda na akaelezea umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na wadau katika kutafuta suluhisho.
“Changamoto ya Tanzania si uzalishaji wa umeme, bali ni usambazaji wa uhakika. Viwanda vingi hupata hasara kubwa kutokana na kukatika kwa umeme, hali inayopunguza ufanisi wa uzalishaji na uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa gharama nafuu,” amesema.
Clarke Energy imekuwa ikisaidia kukuza uzalishaji wa viwandani kwa kutoa mifumo ya kisasa ya nishati na huduma za kiufundi za kuimarisha miundombinu ya nishati nchini.
“Kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Clarke Energy inasambaza mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia gesi asilia, ambayo ni safi na rafiki kwa mazingira ikilinganishwa na dizeli, makaa ya mawe, na vyanzo vingine vya nishati,” ameongeza.
Jani pia amebainisha kuwa kampuni hiyo inatoa mafunzo kwa wateja wake juu ya matumizi bora ya mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, ikiwa ni pamoja na kurejesha joto, mvuke, au baridi kutoka kwa sehemu ya moshi wa mitambo hiyo. Hatua hii pia huchangia kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
“Tunalenga kuchukua hatua madhubuti kuboresha sekta ya nishati Tanzania kwa kushirikiana na mashirika makubwa kama TANESCO na TPDC ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda, taasisi, na jamii,” amesema.
Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Emile Hamman, alisisitiza kuwa kampuni hiyo inalenga kuimarisha sekta ya nishati kupitia ushirikiano na viwanda, wazalishaji wa umeme binafsi (IPPs), na mashirika ya serikali.
“Clarke Energy haina uwekezaji wa moja kwa moja katika miradi ya uzalishaji wa nishati. Badala yake, tunatoa vifaa vya kuzalisha umeme na huduma za baada ya mauzo kwa wateja wetu. Kwa mfano, kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga kilichopo mkoani Lindi ni moja ya maeneo ambapo tumewezesha uzalishaji wa nishati kwa kutumia gesi asilia,” Hamman alieleza.
Hamman pia alieleza mipango ya kampuni hiyo ya kupanua huduma zake katika mikoa yenye shughuli nyingi za viwanda kama Dar es Salaam, Morogoro, na Arusha, huku wakitegemea ushirikiano wa TPDC kuboresha usambazaji wa gesi.
“Kwa kuongeza idadi ya wazalishaji wa viwandani wanaotumia nishati safi, tunalenga kuboresha ufanisi wa kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Tanzania,” aliongeza Hamman.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lodhia Industries Limited, Manoj S. G amesema kampuni yake inanufaika na mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 5 (MW) uliotolewa na Clarke Energy, ikiwa ni pamoja na uhandisi wa awali (FEED), usakinishaji, uzinduzi, na matengenezo endelevu.
“Walifanya utafiti za kina na walifanya juhudi kubwa kuelewa mahitaji yetu. Walifunga hata mifumo ya uchunguzi ili kufuatilia mahitaji yetu ya umeme, matumizi ya kilele na muda wa chini, na masuala mengine ya kiufundi,” alisema Manoj.