Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wajawazito wazingatie mafunzo kupata uzazi salama’

Ofisa Mkuu Mwendeshaji wa Jubilee Health Insuarance, Saleh Shaban (kushoto) na Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Biashara, Masoko na Mawasiliano wa hospitali ya Aga Khan, Olayce Lotha wakimkabidhi mama mjamzito Mariam Rajab, vitabu vya mafunzo.

Muktasari:

  • Wanawake wajawazito wametakiwa kuzingatia mafunzo kabla, wakati na baada ya ujauzito ili kuwa na uzazi salama.

Dar es Salaam. Wanawake wajawazito wametakiwa kuzingatia mafunzo ya utunzaji ujauzito kabla, wakati na baada ya kujifungua ili kuwa na uzazi salama.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Juni 22, 2024 katika mafunzo ya siku moja ya wanawake wajawazito wa jijini hapa yaliyoambatana na uzinduzi wa programu ya 'Safari ya salama ya mama mjamzito' inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Aga Khana na kampuni ya bima ya afya ya Jubilee Health Insurance.

Ofisa Ukuzaji Afya Njema wa Jubilee Health Insurance, Dk Milembe Makoi, amesema wameamua kuleta programu hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanamuangalia mama mjamzito kabla, wakati na baada ya ujauzito wake.

"Tuanze kumuangalia huyu mama tangu anajiandaa kuwa na ujauzito, anapokuwa na ujauzito na baada ya kujifungua na katika programu hiyo tutakuwa tunatoa mafunzo sahihi katika safari yake hiyo ya kupata mtoto na hivyo kusaidia kupunguza pia vifo vitokanavyo na uzazi," amesema Dk Milembe.

Amesema chanzo programu hiyo ni kundi la WhatsApp waliliolianzisha miaka mitatu iliyopita la walilolipa jina la Jubilee Mums Club, ambapo kina mama waliojiunga humo walipata wasaa wa kuuliza maswali na kujibiwa na wataalamu.

"Ndani ya kundi hilo tuna wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa kina mama na wa watoto,  maofisa lishe na maofisa ustawi wa jamii, ambapo kina mama wanapata uwanja mpana wa kujibiwa maswali yao," amesema Dk Milembe.

Hata hivyo, amesema kwa sasa wameona waende mbali zaidi kuwashirikisha na kinamama ambao hawapo mitandaoni na matarajio yao ya baadaye pia kuwafuata wanawake katika vituo vyao vya kiliniki ili kuwafikisha elimu hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Biashara, Masoko na Mawasiliano wa Hospitali ya Aga Khan, Olayce Lotha,  amesema wamefurahishwa na wazo hilo na ndio maana wakashiriki kwa kuamini wanawake wajawazito wanatakiwa kulindwa katika safari yao hiyo kuanzia mwanzo.

Lotha amesema katika kuendelea kuunga juhudi hizo za mama kujifungua salama,  wamewaandalia pia vifurushi mbalimbali ikiwemo kuruhusu kuweka fedha kwa kudunduliza mpaka kufikia hatua ya kujifungua.

"Kujifungua kwa kawaida hapa kwetu ni Sh2 milioni hivyo mama mjamzito anaruhusiwa kuweka fedha kidogokidogo hadi atakapofikia muda wa kujifungua.

"Kwa upande wa kujifungua kwa upasuaji ni Sh4 milioni, lakini hii haina uhakika kwa kuwa katikati ya operesheni kunaweza kutokea mambo mengi hivyo mama anaweza akajikuta anahitajika kutoa fedha nyingine pia," amesema.

Ofisa Mkuu Mwendeshaji wa Jubilee Health Insurance, Saleh Shaaban, amesema programu hiyo haiishi kwa mama anapojifungua tu, bali wanaenda mbali mpaka kwenye kulea watoto wao kuanzia umri sifuri hadi miaka mitano.

"Tunaamini kwa kufanya hivyo tutawasaidia kina mama kupata taarifa mbalimbali ambazo ni sahihi kwa kuwa sasa hivi kutokana na kukua kwa teknolojia,  kuna walimu wengi huko mitandaoni hadi wengine kufikia kudangabya kutokana na kutokuwa na elimu sahihi katika eneo hilo la wajawazito na uleaji wa wato," amesema Shaaban.

Kwa upande wake mama mjawazito, Anneth Lyatuu mkazi wa Kigamboni, amesema program hiyo inamrahisishia gharama za ujauzito.

"Kama mimi hii mimba ni mtoto wangu wa tatu, lakini haijanizuia kuja kuhudhuria mafunzo haya kwa kuwa kila siku vinatokea vitu vipya katika uleaji mimba na kulea watoto," amesema Anneth.

Naye Mariam Said mkazi wa Kinondoni amesema anachotarajia ni kusikia namna ya kumlea mtoto hususani katika suala zima la lishe pamoja na lishe kwa mama kipindi cha chake chote cha ujauzito.