‘Walimu kuwatandika wanafunzi viboko siyo mbinu kufaulu hisabati’

Maadhimisho ya siku ya hisabati duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro, wanafunzi waliohudhuria maadhimisho hayo wakipita kwenye Banda la maonyesho. Picha na Lilian Lucas.
Morogoro. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetakiwa kuelekeza nguvu zake kwenye somo la Hisabati ili kuhakikisha linafanya vyema kuanzia elimu ya msingi.
Aidha imeelezwa kuwa endapo somo hilo litafanya vyema changamoto zilizopo za wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari ama ngazi nyingine za juu wataweza kufanya vizuri na ufaulu kuongezeka tofauti na ilivyo sasa ambapo ni asilimia ishirini tu ya ufaulu ndio imekuwa ikijitokeza kwa zaidi ya miaka ishirini mfululizo.
Mkuu wa idara ya hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sylvester Rugeihyamu amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Hisabati Duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro.
Dk Rugeihyamu amesema katika maendeleo ya hisabati Tanzania changamoto bado ni kubwa katika ufaulu ukilinganisha na masomo mengine. Hivyo jitihada za ziada zinatakiwa kuchukuliwa kuanzia Serikali, walimu na wazazi kwani hisabati ni msingi wa masomo yote na maboresho ya ufundishaji yanahitajika pia kwa walimu.
“Kinachotakiwa ni jitihada ya Serikali kuliona tatizo lililopo na ukiendelea hivi ni kwamba kutakuwa na wataalamu wachache ambao wataweza kumudu masuala ya kisayansi, sehemu nyingi za kimaisha. Kwa hiyo kati ya watu 100 asilimia tulionayo 20 ndio wanapita 80 ni kwamba uwezo wao ni mdogo sana jambo ambalo ni hatari,”amesema.
Aidha malengo makuu ya serikali ni kujenga Serikali ya uchumi wa viwanda katika teknolojia, utaratibu uliopo wa ufundishaji unatakiwa kubadilika kuanzia ufundishaji, na mategemeo ya miaka kumi ijayo Tanzania lazima itabadilika na kwenda kwenye teknolojia ya kisasa na kuachana na utaratibu uliopo sasa wa mazoea.
“Ushauri wangu kwa serikali ni kuweka msingi katika shule za msingi, kuwe na mkazo zaidi watoto wawe na ushawishi wa uelewa, matokeo tunayoyaona kwenye sekondari ni matatizo yanayozalishwa kutoka kwenye shule za msingi. Shule za msingi zina matatizo yake kuna walimu wengi wanajari kwamba kila mwalimu yoyote anaweza kufundisha hisabati kitu ambacho si kweli, kuna mwalimu alikimbia hisabati leo unamwambia afundishe. Serikali itoe kipaumbele katika somo la hisabati kwani kuna walimu wachache na wana mzigo mkubwa kufundisha,”amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita), Betinasia Manyama amehimiza wanafunzi, wazazi na walimu kuhusu somo hilo ambapo aliwataka walimu wakati wa kufundisha somo hilo kuacha kutumia viboko na badala yake wawafanye kuwa marafiki ili wanafunzi waweze kulipenda.
Manyama amesema malengo ya maadhimisho hayo ni kuboresha mbinu mbalimbali za ufundishaji, kuwajengea uwezo walimu kukabiliana na darasa lenye wanafunzi wengi na kuongeza hamasa kwa walimu wa hisabati hata katika changamoto za uhaba wa walimu.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro anayeshughulikia Elimu, Germana Mung’aho akizungumza katika maadhimisho hayo, amesema pamoja na kwamba somo la hisabati lina changamoto katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi zote za elimu akapongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Chahita katika kuhamasisha jamii wakiwemo wanafunzi, walimu na wadau wengine wa elimu.
Aidha Mung’aho alisema ujenzi wa taifa lenye uchumi imara na maendeleo endelevu hauwezi kufikiwa kama ufaulu wa somo la hisabati uko chini, kwani hisabati ni msingi wa maendeleo kwa nyanja mbalimbali kama sayansi na teknolojia, viwanda, fedha, madini, kilimo,maji na takwimu.
Mwaka jana 2022 ufaulu wa Hisabati kwa darasa la saba ni asilimia 53.29 na kidato cha nne ni asilimia 20.08.