Waziri Mkuu asitisha utoaji vibali vya uvunaji mbao
Muktasari:
Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya kupandwa 18, na kati ya hayo uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba nane ambayo ni Sao Hill (Mufindi), Buhindi (Sengerema), Meru/Usa (Arumeru), West Kilimanjaro (Hai), Shume (Lushoto), North Kilimanjaro (Rombo), Kiwira (Rungwe) na Kawetire (Mbeya Vijijini).
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesitisha utoaji wa vibali vya uvunaji wa mbao kutoka katika mashamba nane ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya kupandwa 18, na kati ya hayo uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba nane ambayo ni Sao Hill (Mufindi), Buhindi (Sengerema), Meru/Usa (Arumeru), West Kilimanjaro (Hai), Shume (Lushoto), North Kilimanjaro (Rombo), Kiwira (Rungwe) na Kawetire (Mbeya Vijijini).
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana na kufafanua kwamba usitishaji huo unalenga kutathmini taratibu, kanuni na vigezo sahihi vinavyotakiwa kutumika katika kugawa malighafi kutoka kwenye mashamba hayo.
Amesema wadau wote wa viwanda vinavyojikita katika malighafi ya misitu na hususan wamiliki wa viwanda vya kupasua mbao wanashauriwa kuwa watulivu wakati utaratibu huu ukifanyiwa mapitio na umma utatangaziwa rasmi pindi uboreshaji huo utakapokamilika.