161 wadakwa Kilimanjaro kwa tuhuma mbalimbali
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa
Muktasari:
- Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wanawashikilia watu 161 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali ikiwemo kutengeneza gongo lita 200, bangi misokoto 2280 na kukutwa na mirungi kilo 310.
Moshi. Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wanawashikilia watu 161 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali ikiwemo kutengeneza gongo lita 200, bangi misokoto 2280 na kukutwa na mirungi kilo 310.
Pia walikutwa na pikipiki 1404 zilizokamatwa katika opereseheni maalumu inayoendelea mkoani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa ndani ya siku saba katika opresheni maalumu inayoendelea mkoani humo.
Amesema miongoni mwa waliokamatwa 132 wamefikishwa mahakamani na wengine 29 uchunguzi unaendelea dhidi yao.
Polisi pia wanawashikilia watuhumiwa sita wa kosa la kuwajeruhi kwa mawe na fimbo waumini wa dini ya Kiislam waliokuwa kwenye sherehe ya maulid iliyokuwa ikifanyika katika kijiji cha Maore chini kata ya Ndungu wilayani Same.
"Baada ya tukio hilo kufanyika watuhumiwa walikimbia na baadaye msako mkali ulifanyika na tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita, "amesema Kamanda Maigwa.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa uongozi wa msikiti uliopo katika kata hiyo.