ACT Wazalendo yaahidi kurejesha mamlaka kamili Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Jadida Wete Pemba

Pemba. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud amesema visiwa hivyo kushindwa kujiamulia mambo yake ni sawa na kunyang’anywa mamlaka zake za fedha, kodi na kukopa kimataifa.

Ametoa kauli hiyo leo Juni 11, 2023 katika muendelezo wa ziara za chama hicho katika Uwanja wa Jadida Wete, Pemba na kuwasisitiza wanachama, wafuasi na wananchi wote bila kujali itikadi zao za vyama kuungana kudai mamlaka ya Zanzibar.

"Tuamue kama tunataka muungano sawa kama hatuutaki si dhambi maana si faraji wa suna tunatakiwa tupate mamlaka kamili na haya hatuyasemi kwa kificho," amesema

Amesema nia ya chama hicho ni kuhakikisha wanajenga Zanzibar mpya, Zanzibar moja na yenye mamlaka kamili kwani bila hivyo kwa mujibu wa Othman ni ndoto taifa hilo kujiondoa katika wimbi la umasikini.

Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salim Bimani amesema hakuna usafiri wa uhakika katika kisiwa hicho na kuitaka Serikali kuhakikisha inaimarisha usafiri huo ili kuepusha madhara ambayo yamekuwa yakitokea kutokana na kadhia hiyo.

Mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Ismail Jussa amesema wakati umefika chama hicho kushika dola ili kuleta utawala wa haki na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma kama ilivyo sasa kulingana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Jussa ametoa kauli hiyo akirejea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilibainisha dosari na kuonyesha upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha zikiwemo zile zilizotolewa Kwa ajili ya kupunguza ahueni ya Uviko-19 ambapo Zanzibar ilipewa Sh230 bilioni

Mkutano huo ni muendelezo wa Mikutano ambayo Chama hicho kimeitambulisha kuwa ni 'Darasa' la kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi juu ya changamoto na masaibu ambayo yanawakabili, na wajibu wa kuendelea kuyapazia sauti ndani ya Nchi yao, sambamba na kuifikisha ile dhana ya ''Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja yenye Mamlaka Kamili'', kwa watu wote.