ACT yalaani kukamatwa viongozi wa Chadema

Muktasari:
- Ngome ya vijana ACT-Wazalendo inalaani vikali tukio la kukamatwa viongozi a Chadema huko Mwanza.
Dar es Salaam. Ngome ya vijana ACT-Wazalendo inalaani vikali tukio la kukamatwa viongozi a Chadema huko Mwanza.
Hayo yamesemwa leo Julai 22, 2021 na Katibu Itikadi na Uenezi ngome ya vijana ACT, Julius Massabo katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo amesema suala hilo siyo dhidi ya Chadema tu, bali ni dhidi ya demokrasia.
Amesema watu kukusanyika ndani kujadili juu ya madai ya Katiba mpya haiwezi kuwa jinai kwani sheria na Katiba ya nchi vinaruhusu.
"Tafsiri ya tukio lililotokea Mwanza la kukamatwa kwa viongozi wa Chadema ni ujumbe kwetu kwamba wananchi kujadili au kudai Katiba mpya ni kosa la jinai, kukalia kimya jambo hili ni kuruhusu Katiba na sheria kuendelea kukanyagwa," alisema Massabo.
Amesema Katiba mpya ni hitaji la wananchi hivyo haipaswi kuwa takwa la kiongozi wa Serikali.
Amesisitiza mapambano dhidi ya Katiba mpya si lelemama na inahitaji ushiriki wa watu wote.
"Mapambano dhidi ya Katiba mpya ni ya wananchi, vyama vyote vya siasa, wataalamu mbalimbali pamoja na viongozi wa dini," alisema.