Adaiwa kumnyonga mkewe, naye ajinyonga

Muktasari:

 Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amesema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mwanaume huyo alitekeleza tukio hilo la mauaji ya mkewe na baadaye kujinyonga mwenyewe.

Kigoma. Mkazi wa mtaa wa Gemu, kata ya Mwanga Kusini, Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma, Rashid Mkayala(38), anadiwa kumuua mkewe , Benadetha Cosmas(34), kwa kumnyonga shingoni hadi kufa na kisha na yeye kujinyonga kwa kutumia kitambaa cha kichwani,   huku chanzo ni ugomvi baina yao baada ya mke kumtuhumu mume kuuza vitu vya ndani ikiwemo chakula.

Tukio hilo limetokea  jana Februari 21,2024  baada ya majirani na ndugu kuvunja milango ya nyumba ya wanandoa hao ambapo waliweza kuona miili yao wakiwa tayari wameshafariki dunia.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amesema uchunguzi wa awali,  ulibaini kuwa mwanaume huyo alitekeleza tukio hilo la mauaji ya mkewe na baadaye kujinyonga mwenyewe.

“Hadi tukio hilo linatokea wanandoa hao walikuwa kwenye ugomvi wa mke kumtuhumu mumewe kuuza vitu vya ndani, ambapo mwanaume huyo alimnyonga kwa mikono mkewe hadi kufa na baadaye na yeye akajiua kwa kutumia kitambaa kwa kujitundika kwenye kenchi ya nyumba.

Amesema miili yao imehifadhiwa katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni kwa uchunguzi zaidi,”

Naye mdogo wa marehemu Benadetha, Isaac Cosmas amesema siku moja kabla ya tukio ilikuwa muda wa saa tatu asubuhi dada yake alimpigia simu na kumuomba aweze kwenda nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa.

Amesema  alipofika nyumbani kwa mwenyekiti , alianza kumhadithia kuwa amelala kwa mwenyekiti kumkimbia mumewe baada ya kumpiga sana kwa kutumia waya wa kuunganisha televisheni na king’amuzi na kumuumiza vibaya na alipopata nafasi aliweza kutorokea nyumbani kwa mwenyekiti huyo.

“Baada ya kuzungumza nilimchukua tukaenda hadi nyumbani kwake na kukutana na mumewe na kwa pamoja niliwasikiliza na kila mmoja kutambua kosa lake na kuwaomba wasiendeleze ugomvi na badala yake waishi kwa amani,”amesema  Cosmas.

Amesema  kwa maelezo ya dada yake kabla ya tukio hilo aliwamwambia anadai talaka yake kwani amechoka kuishi na huyo mwanamume,  kutokana na kumpiga mara kwa mara na hadi kumtishia kumnyonga kwa kutumia kamba ya chaja ya simu.

Mtoto wa marehemu, Hussein Rashidi amesema wazazi wake walikuwa wakigombana mara kwa mara huku mama yake alikuwa akikimbia nyumbani na kulala kwa viongozi wa serikali wa  mtaa huo, kutokana na vipigo alivyokuwa akipigwa na baba yake.

Jirani  Ally Mohammed amesema anamfahamu marehemu Rashidi tangu  ameanza kuishi mtaa huo hakutegemea kuwa atakuwa na roho ya aina hiyo ya kuweza kumuua mkewe na yeye kujiua.

‘’Ukimwangalia huwezi kudhani kama anaweza kufanya tukio kama hilo ndio maana  kila mmoja amepata mshtuko wa tukio hilo,’’ amesema.

Naye Mariamu Ibrahim amesema tukio hilo limewasikitisha sana wao kama majirani, kwani  kama wanandoa wakiona wameshindwa kuishi pamoja,  ni bora wakaachana kuliko kufikia hatua ya kuuana.