Adaiwa kumuua kaka yake baada ya kutomlipa Sh700,000

Adaiwa kumuua kaka yake baada ya kutomlipa Sh700,000

Muktasari:

Polisi wilaya ya Serengeti wanamshikilia Juma Masiaga (38) mkazi  wa kijiji cha Kitunguruma kwa tuhuma ya kumchinja kaka yake, Chacha (40) kwa madai ya kutomlipa Sh700,000.

Serengeti. Polisi wilaya ya Serengeti wanamshikilia Juma Masiaga (38) mkazi  wa kijiji cha Kitunguruma kwa tuhuma ya kumchinja kaka yake, Chacha (40) kwa madai ya kutomlipa Sh700,000.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Desemba 24, 2020 mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema tukio hilo limetokea jana saa nne usiku.
"Alimvizia na kumkata shingoni na kichwani kisha akakimbia na leo amenaswa eneo la jalala kuu mjini Mugumu akijaribu kutoroka, sasa anahojiwa na polisi kwa ajili ya hatua zaidi," amesema.

Amesema taarifa zilizopo ni kuwa alikuwa akimdai kaka yake Sh700,000 baada ya awali kulipwa Sh800,000.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Joseph Petro amesema hakuwahi kusikia mgogoro wowote  wa ndugu hao na kwamba kama alikuwa na malalamiko angeyawasilisha sehemu husika.