Ado aitaka Serikali kutatua changamoto ajira kwa vijana
Muktasari:
Katibu mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema ni wajibu wa Serikali kuzalisha ajira kwa vijana ili kulinda haki zao katika Taifa.
Dar es Salaam. Katibu mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema ni wajibu wa Serikali kuzalisha ajira kwa vijana ili kulinda haki zao katika Taifa.
Ado ameyasema hayo leo Januari 14 alipohutubia kongamano la ngome ya vijana chama hicho jijini Dar es Salaam lililokuwa na mada isemayo, ‘Ukiukwaji wa haki za vijana.’
Ado aliyezindua kalenda ya ACT Wazalendo iliyoandaliwa kwa utashi na ubunifu kutoka ngome ya vijana ya chama hicho, pia ameitaka jamii kupigania haki za vijana, hususani ukosefu wa ajira ili kuinua uchumi na kupambana na umasikini.
"Mazingira ya ajira ni magumi sana kwa vijana wetu, hali ambayo inasababisha uchumi kuwa mbaya, kwa hiyo kama ajira hazipo hiyo ni dalili za kufeli kwa Serikali.
“Vijana tunatakiwa kupigania ndoto zetu Ili kufika mahali ambapo tuna stahili kufika,” amesema.
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa ngome ya vijana kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Felix Kamugisha amesema kwa utashi waliokuwa nao wameona kuna umuhimu wa chama kuwa na kalenda yao maalumu kama alama ya chama.
Ameongeza kuwa, "vijana ndio chachu ya mabadiliko mbalimbali katika nchi, hivyo vijana wakitambua haki zao kutakua na maendeleo tofauti katika jamii."
Naye Katibu mkuu ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Twaha Rashid, amesema anatamani kuona vijana wanachangamkia fursa katika masuala ya siasa kwa kuwa ni jambo la msingi kwao.
"Vijana amkeni sasa kumekucha, siasa ni jambo la msingi sana kwenu katika maendeleo ya taifa lenu baadaye," amesema.
Katibu wa ngome ya Vijana Taifa kutoka ACT Wazalendo, Mwanaisha Mdeme amesema ni wakati wa vijana kushiriki katika uamuzi wa masuala mambalimbali ambayo yamekua yakileta tija katika jamii.
"Tunatakiwa kujenga Taifa lenye vijana imara wanaoweza kufanya maamuzi na kuibadilisha jamii kwa ajili ya maendeleo mbalimbali" amesema
Naye mgeni mwalikwa ambaye ni Mwenyekiti wa vijana Taifa kutoka chama cha NCCR, Mageuzi Frank Rungwana amesema vijana wanatakiwa kuzungumzia masuala yanayowahusu na yenye kuleta mageuzi katika jamii.
"Kama vijana tunatakiwa kuongelea masuala yanayotuhusu na yenye kuleta mabadiliko katika jamii zetu," amesema.
Grace Michael ambaye ni kijana kutoka Segerea amesema wao kama vijana anaamini wanaweza kusimamia haki zao wenyewe, hivyo anawaasa vijana wenzake kutokukubali kuyumbishwa katika mambo ya msingi na yenye tija.
"Tukiwa kama vijana wenye nia ya kuibadilisha taifa letu tunatakiwa kusimamia imara huku tukiyafuta yale yatakayo weza kuleta mabadiliko katika jamii zetu" amesema.