Ahadi ya Serikali kwa wakulima wa miwa
Muktasari:
- Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wakulima wa miwa wanapata masoko ya uhakika.
Moshi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wakulima wa miwa wanapata masoko ya uhakika.
Ameeleza hayo leo Jumanne Machi 2, 2021 alipotembelea kiwanda cha sukari TPC kuangalia shughuli za uzalishaji za kiwanda hicho.
"Tutahakikisha wakulima wa miwa wanapata masoko ya uhakika, kuna changamoto ya wakulima wa miwa walioshindwa kuuza miwa yao, naomba niwahakikishie tutamaliza changamoto hii ili tuongeze uzalishaji wa sukari nchini," amesema Profesa Mkenda
Ameupongeza uongozi wa TPC kwa kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 36,000 hadi 110,000 kwa mwaka.
"Serikali tulivyobinafsisha viwanda vya sukari vya TPC, Mtibwa ,Kagera na Kilombero wote waliopewa vile viwanda walipewa viwango vya kuongeza uzalishaji ambapo kiwanda hiki ndio kimetimiza na kupitiliza yale malengo yaliyowekwa.”
"Nimefurahi sana kuona kiwanda hiki kinavyofanya kazi kimetimiza na kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 36,000 hadi 110,000 kwa mwaka na mwaka huu serikali tumepata gawio la Sh15.5 bilioni," amesema Profesa Mkenda.
Jafary Ally , ofisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho amesema wamekuwa na mafanikio makubwa ya uzalishaji wa sukari kutoka tani 36,000 hadi 110,000 kwa mwaka.
"Mwaka huu tumefanikiwa kuzalisha tani 103,000 licha ya kwamba mwaka jana tulipata changamoto ya mafuriko," amesema Ally.