Ajinyonga kwa madai ya kuzidiwa madeni ya Vikoba

Muktasari:

  • Mkazi wa Kihesa Kilolo, Manispaa ya Iringa Enea Mkimbo amejinyonga kwa kutumia kitenge kwa madai ya kuzidiwa na madeni ya vikoba.

Iringa. Mkazi wa Kihesa Kilolo mkoani Iringa, Enea Mkimbo (55) amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge kwa madai ya kuzongwa na madeni ya Vikoba.

 Inadaiwa jana Septemba 13, 2022 wanakikundi wenzake walienda nyumbani kwake kudai madeni na ilipofika jioni akamuaga mumewe, Edward Sanga kuwa anakwenda nyumbani kwa mama yake mzazi na badala yake aliingia jikoni na kujitundika kitanzini hadi kufa.

Leo Septemba 14, Mwananchi imeshuhudia msiba wa Enea ukitengwa kwenye nyumba mbili kutokana na mvutano ulioibuka baina ya upande wa kike na kiume wakidai, hakulipiwa mahari.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha tukio hilo na kwamba, wanaendelea na upelelezi kuhusu madai ya Enea kujiua.

“Tukio limetokea na ni kweli marehemu alikuwa anadaiwa madeni ya Vikoba na wenzake, tunaendelea na upelelezi tutatoa taarifa kamili,” amesema Bukumbi.

Baadhi ya ndugu na majirani wakiwa kwenye msiba nyumbani kwa Enea Mkimbo, aliyejinyonga kwa madai ya kuzongwa na madeni ya vikoba

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kihesa Kilolo B, Michael Mlalwe amesema alipigiwa simu ya Enea kujinyonga saa 12 asubuhi na kutoa taarifa polisi ambao walikuja kuchukua mwili.

“Inasemekana ni madeni ya Vikoba na jana wenzake walikuja kumdai lakini hatujui zaidi. Changamoto tunayohangaika nayo sasa ni eneo la msiba. Wananchi wa Kihesa, Kilolo na mume wanataka msiba uje nyumbani kwa marehemu na upande wa kike wametenga msiba huko,” amesema Mlalwe.

Mume wa marehemu, Sanga amesema “Naomba mke wangu aletwe nyumbani, hiki kibanda tulijenga wote yeye anasomba maji mimi najenga, aje nimuage. Hapa ni nyumbani kwangu na ni mke wangu,” amesema na kuongeza;

“Nilituma washenga mara mbili walikataa kupokea posa, tuna watoto na wajukuu, nitalilia hapa,” amesema.

Kaka wa marehemu, Aldo Chonya amesema mama mzazi wa marehemu ameagiza kuwa msiba utengwe nyumbani kwake na yeye hataondoka kwenda kulia sehemu nyingine.

“Na sisi tumepokea msiba kama mlivyosikia kuwa amejinyonga, sababu hatujui lakini mama amesema msiba utakuwa hapa,” amesema Chonya.