Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ajiua kwa kunywa sumu, kisa kufiwa na wajukuu watatu maporomoko Rungwe

Muktasari:

  • Maporomoko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Machi 25 mwaka huu, kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika kata za Lupepo, Kinyala, Ikuti, Kawetele na Nkunga. Tukio hilo limesababisha vifo vya watu 21, wakiwemo watoto 14.

Mbeya.  Simanzi, huzuni na taharuki vimetanda katika Kijiji cha Mboyo, Kata ya Ikuti, Wilaya ya Rungwe, baada ya mkazi wa eneo hilo, Hamis Mwasomola (65), kujitoa uhai kwa kunywa sumu ya kuua magugu kufuatia mshtuko wa kupoteza wajukuu wake watatu.

Tukio hilo limetokea Machi 26, mwaka huu, siku moja baada ya maafa ya maporomoko ya tope yaliyofunika nyumba za familia 11 katika kata za Nkunga, Kinyala, Ikuti, Lupepo na Kawetele wilayani humo, na kusababisha vifo vya watu 21 papo hapo, wakiwemo watoto 14.

Inaelezwa kuwa maporomoko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Machi 25, 2025, majira ya saa sita usiku, kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha kwa takribani saa nne mfululizo.


Simulizi ya familia

Mdogo wa marehemu, Elia Mwasomola amesema familia imepata pigo kufuatia matukio hayo mawili yaliyotokea ndani ya muda mfupi.

Alisema siku ya tukio, marehemu alipata msongo mkubwa wa mawazo baada ya kushuhudia miili ya wajukuu zake watatu eneo la tukio, na kuhofia kuwa mwanawe wa kiume, ambaye ni tegemezi wa familia, naye angekuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

“Siku ya tukio alifika eneo la maporomoko na kushuhudia miili ya wajukuu zake watatu. Baadaye alitoweka ghafla na hatukujua alipoelekea,” alisema.

Alisema kutoweka kwake kulizua taharuki na juhudi za kumtafuta zilianza mara moja hadi walipofika nyumbani kwake na kukuta mlango umefungwa kwa ndani.

“Haikuwa kawaida yake kujifungia ndani. Tuliposukuma mlango, tulimkuta tayari amekunywa sumu ya kuua magugu. Tulimpeleka hospitali ya jirani, lakini alifariki dunia licha ya jitihada za madaktari,” alieleza.

Kwa mujibu wa Elia, kabla ya kufariki dunia, marehemu alieleza kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na maumivu makali ya kupoteza wajukuu wake, yaliyomwathiri kisaikolojia.

“Nikiwa namuuguza, aliniambia hawezi kuvumilia maumivu aliyokuwa nayo baada ya kupoteza wajukuu zake. Ingawa baadaye alionekana kujutia uamuzi wake,” alisema.

Aliongeza kuwa familia hiyo pia ilifiwa na mama yao mzazi mwezi uliopita, jambo lililoongeza uzito wa majonzi wanayopitia kwa sasa.

Mtoto wa kwanza wa marehemu, Lainess Hamis (40), alisema wanaamini baba yao alichukua uamuzi huo baada ya kushindwa kuvumilia maumivu ya kuona miili ya wajukuu wake.

“Bado tunaumizwa na tukio hili. Alifika eneo la tukio, kisha akaondoka bila kusema chochote. Baadaye tulipigiwa simu kuwa amekunywa sumu,” alisema.

Aliongeza kuwa marehemu aliacha ujumbe mfupi akiagiza baadhi ya mali zake zigawiwe, likiwemo shamba la karanga na Sh5,000 apewe ndugu aliyekuwa akiishi naye.

Kufuatia maafa hayo, Spika mstaafu na Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson, Aprili 1, 2026, alifanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathirika, kuwapa pole waathirika na kukabidhi msaada wa mchele kilo 440 pamoja na Sh4.4 milioni kwa familia zilizoathirika.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Dk Tulia alisema athari za maafa hayo bado ni kubwa, na familia nyingi zilipoteza makazi na kulazimika kuishi kwa majirani.

Alisema lengo la ziara yake ni kujionea hali halisi pamoja na kutoa pole na faraja kwa familia 11 zilizokumbwa na janga hilo, akibainisha kuwa mahitaji bado ni makubwa na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia.

“Tumetembelea familia katika kata za Lupepo, Kinyala, Ikuti, Kawetele na Nkunga. Hali siyo nzuri, wengi wamepoteza makazi na wanaishi kwa majirani. Kuna uhitaji mkubwa wa chakula, magodoro na makazi bora,” alisema.

Alifafanua kuwa mgao wa msaada huo umezingatia idadi ya waliopoteza maisha katika kila familia, ambapo familia iliyopoteza mtu mmoja hupatiwa Sh200,000 na kilo 20 za mchele, huku kiwango kikiongezeka kulingana na idadi ya vifo.


Kauli ya CCM

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe, Mekson Mwakipunga alisema tukio hilo limeacha majonzi makubwa kwa wakazi wa eneo hilo, huku baadhi ya familia zikipoteza makazi kabisa.

“Katika Kijiji cha Mboyo, familia moja imepoteza wajukuu watatu. Ni tukio la kusikitisha ambapo babu yao aliamua kujitoa uhai baada ya kushindwa kuvumilia maumivu ya kisaikolojia,” alisema.

Alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kuendelea kutoa msaada kwa waathirika wa maafa hayo ili kuwasaidia kurejea katika hali ya kawaida.