Akamatwa nchini Austria akidaiwa kukutwa na vinyonga 74 kutoka Tanzania

Akamatwa nchini Austria akidaiwa kukutwa na vinyonga 74 kutoka Tanzania

What you need to know:

  • Mtu mmoja ambaye hajatambuliwa jina lake amekamatwa nchini Austria akitorosha vinyonga 74 kutoka Tanzania.

Dar es Salaam. Mamlaka nchini Austria zimemkamata mtu mmoja katika uwanja wa ndege wa Vienna akiwa anatorosha vinyonga 74 kutoka nchini Tanzania.

Taarifa kutoka nchini humo zilizoandikwa katika gazeti la The Telegraph la Uingereza zinasema mtu huyo mwenye umri wa miaka 56 ambaye hakutambuliwa zaidi alikuwa amewaficha wanyama hao katika soksi na masanduku ya barafu alipokamatwa na maofisa forodha wa uwanja huo wa Vienna.

Naibu katibu mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii  nchini Tanzania, Allan Kijazi amesema wanazo taarifa kuhusu kukamatwa kwa mtu huyo na wanafuatilia.

“Alisafiri kwenda Austria kutoka Tanzania kupitia Ethiopia,” limeeleza gazeti hilo na kubainisha kuwa vinyonga hao walikuwa wakipelekwa kwenye bustani ya wanyama ya Schoenbrunn na ilibainika kuwa  watatu wamekufa.

 “Wanyama wote walikuwa wanatoka katika milima ya Usambara Tanzania na walikuwa katika umri wa wiki moja hadi wakubwa,” limeeleza gazeti hilo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika masoko ya ulanguzi vinyonga hao wangeuzwa kati ya Euro 37,000 au Pauni 32,860 sawa na Sh104.12 milioni.