Akutwa amefariki kwenye shamba la mifugo

Muktasari:

Mkazi wa Kijiji Cha Mwanangwa Kata ya Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Juma Shilatu (40) amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na walinzi wa Suma JKT katika shamba la uzalishaji mifugo la Mabuki walilokuwa wakililinda kisha kukamata ng’ombe 20 alizokuwa akichunga.

Misungwi. Mkazi wa Kijiji Cha Mwanangwa Kata ya Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Juma Shilatu (40) amefariki dunia kwa madai ya kupigwa na walinzi wa Suma JKT katika shamba la uzalishaji mifugo la Mabuki walilokuwa wakilinda kisha kukamata ng’ombe 20 alizokuwa akichunga.

Mmiliki wa Ng'ombe alizokuwa akichunga, Sungano Degeleka (56) mkazi wa Kijiji Cha Mwanangwa amesema Aprili, 25 mwaka huu jioni, Shilatu akiwa na wenzake wakichunga ndani ya shamba hilo walikutwa na walinzi hao, wenzake walifanikisha kuondoa mifugo yao baada ya mapambano lakini yeye hakufanikiwa.

Degeleka amesema Aprili 26, 2023 wananchi wa Kijiji Cha Mwanangwa waliingia kwenye shamba hilo kumtafuta Shilatu na kumkuta ameuawa akiwa na jeraha kubwa tumboni na kichwani.

“Kijana huyo (Juma Shilatu) ana miaka miwili tangu aanze kuishi nyumbani kwangu na alikuwa akifanya shughuli za kilimo na kuchunga  mifugo.Juzi alikwenda kuchunga kwenye shamba la Mabuki na Ng'ombe zangu 20 zilikamatwa na mchugaji hakurudi nyumbani. Siku iliyofuata tulimkuta ameuawa baada ya kupigwa na walinzi wa shamba hilo,”

“Nilifuatilia ng'ombe zangu 20 zilozokamatwa baadaye siku hiyo (Aprili 26) nilimtuma kijana wangu, Deus Samson (32) kwenda kuzilipia kila ng'ombe Sh120,000 sawa na Sh2.4 milioni kwa ng’ombe zote,” amesema Degeleka

Ofisa mtendeji wa Kijiji Cha Mwanangwa,  Michael Samson amesema alipigiwa simu na Mwenyekiti wa kitongoji Cha Mwabomba Kijiji Mwanangwa, Amosi Lumalasabo  kumweleza kuwa Kuna mtu amekutwa ameuawa na yeye kutoa taarifa kwa viongozi wenzake pamoja na polisi.

Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Mitindo Misungwi, Dk  John Nyasebwa amekiri kupokea mwili wa Shilatu akidai uchunguzi bado haujafanyika.

Meneja wa shamba la uzalishaji mifugo la Mabuki, Lini  Mwala  amesema hana taarifa ya yeyote kuuawa akidai kuna wananchi walienda kuchukuwa ng'ombe 20 na kulipa faini kama taratibu zao zinavyosema.

“Kwa taratibu zetu huwa anatakiwa mchugaji aje kuzichukua yeye, tuliwauliza mchugaji wa ng'ombe yuko wapi wakasema yupo nyumbani nashangaa kusikia mchugaji ameuawa,”amesema

Diwani wa Kata ya Mabuki, Malale  lutonja amesema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili wananchi wa kata yake wameuawa kwa kupigwa na walinzi wa shamba hilo huku  mmoja aliyepigwa risasi akipata ulemavu .

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema mwili wa Shilatu umepelekwa hospitali ya wilaya hiyo kwa ajili ya uchunguzi.