Alichokisema Majaliwa kuhusu uvaaji wa barakoa

New Content Item (2)
Alichokisema Majaliwa kuhusu uvaaji wa barakoa

Muktasari:

  • Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema barakoa husaidia kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, hasa watu wanapokuwa wamekaa karibu.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema barakoa husaidia kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, hasa watu wanapokuwa wamekaa karibu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Februari 20, 2021 alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga.

“Barakoa unaivaa pale anapojua shughuli zako za siku hiyo zitakupelekea kupata huduma au kutoa huduma na mwingine aliyeko umbali wa chini ya mita moja ambapo panapunguza hatari ya kutema mate au unyevunyevu, hapo sasa unaweza kuvaa. Hakuna aliyekataza. Muhimu kila mmoja aende kwa tahadhari,” amesema Majaliwa.

“Barakoa hizi tunazovaa wakati ule tulisema ni bora tujiridhishe zimetoka wapi. Bora ukatengeneza ya kwako au iliyotengenezwa tanzania...,barakoa ni kinguo tu kinachozua mate yasije yakatoka au ukapokea vitu vingine,” amesisitiza.

Huku akiwataka Watanzania kuwa watulivu, Majaliwa amesema, “mmesikia wote kwenye mitandao kila  mmoja anasema lake. Wale wenye simu zenye taarifa tumeona mataifa mbalimbali huko yakieleza kwamba hii ni vita na ni vita imeanza kwa mataifa makubwa huko bado wanahangaika nayo. Sisi mataifa madogo lazima tuwe makini.”

Huku akimsifu Rais John Magufuli kwa kupambana na ugonjwa huo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuchukua tahadhari kwa kufuata masharti ya afya.