Alikiba, Diamond, Harmonize kimeumana huko!

Saturday June 26 2021
alikibapic
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Haijawahi kutokea, hii ndio mara ya kwanza kwa wasanii watatu wa kubwa wa Bongofleva, Alikiba, Diamond Platnumz na Harmonize kuachia nyimbo kwa wakati mmoja. Ukisikia; Kimeumana, ndio hii sasa.

Juzi jioni Alikiba alianza kuachia wimbo wake 'Salute' akimshirikisha Rudeboy wa Nigeria aliyekuwa akiunda kundi la P Square, jana asubuhi Diamond naye akatoa wimbo 'Kamata', kufika jioni naye Harmonize akaja na ngoma yake iitwao Sandakalawe.

Ujio wa ngoma hizi tatu ndani ya saa 24 kukuleta maneno kutokea kwenye timu za wasanii hawa, wengine wakidai kuna ambaye alitoa kwa lengo la kufunika wimbo wa mwenzake, huku propanda za chini kwa chini zikiendelea.

Hilo likamuibua Diamond ambaye ameonyesha kukerwa na kile achodai kuna watu wanachonganisha wasanii ili wagombane na kuwataka kuwasaidia ili wakashindane kimataifa.

"Mnapoteza muda mwingi sana kwenye kuchonganisha wasanii wenu wa Tanzania ili wagombane, badala ya kutumia muda huo kuwatangaza ili tukashindane na wenzetu wa mataifa mengine na kuleta heshima katika taifa letu, aibu" ameandika Diamond Insta Story.

Hata hivyo Rapa Nay wa Mitego ameishangaa kauli hiyo ya Diamond kwa kumueleeza kuwa ndio mambo ambayo amekuwa akiyapendelea kwenye muziki wake, hivyo awe mpole.

Advertisement

"Ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo, sasa unalia nini wakati ndio huwa unapanda hizi mambo, pambana na hali," amesema Nay wa Mitego kutokea Free Nation.

Haikuchukua muda Harmonize akaijibu kauli ya Diamond ikiwa tayari kaachia wimbo wake, Sandakalawe, "Wachonganishi wote tukutana YouTube only, haya wachonganishi wote tukatane YouTube Konde Boy say so".

Naye Alikiba ambaye ndiye chanzo cha hayo yote hakuwa na mengi zaidi ya kutumia ukurasa wake wa Instagram kutoa ujumbe mfupi kuhusu hilo; "Sema kimeumana kwa sauti" aliandika.

Ikumbukwe wasanii hawa watatu wamekuwa katika ushindani kutokana Diamond ndiye aliyemtoa Harmonize ambaye baadaye alikimbia kwenye lebo yake ya WCB Wasafi na kwenda kuanzisha yake, Konde Music Worldwide. Huku ikidaiwa Alikiba haelewani na Harmonize kutokana alichukua wasanii wake wa Kings Music, Cheed na Killy na kuwasaini katika lebo yake.

Advertisement