Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyehukumiwa miaka 15 kwa kukutwa na heroini aachiwa huru

Muktasari:

  • Nassor Khamis alikamatwa Desemba 3, 2019 katika eneo la Fuoni Kwa Mabala, Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar, akiwa na gramu 15.6211 za heroini.

Arusha. Mahakama ya Rufaa Tanzania imemwachia huru Nassor Said Khamis, aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kukutwa na gramu 15.6211 za dawa za kulevya aina ya heroini.

Mahakama imeeleza kuwa uamuzi huo umetokana na kushindwa kwa upande wa mashtaka kueleza sababu za msingi za kumchelewesha mrufani kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kumfikisha mahakamani, licha ya uchunguzi wa vielelezo kukamilika ndani ya siku chache baada ya kukamatwa kwake.

Imeeleza kuwa ucheleweshaji huo ulidhoofisha uaminifu wa ushahidi wa mashahidi wa mashtaka na kuacha mashaka yaliyopaswa kumpa faida mshtakiwa.

Katika hukumu iliyotolewa Juni 22, 2026, na jopo la Majaji wa Rufaa Barke Sehel, Issa Maige na Lameck Mlacha, Mahakama imesema haikupata maelezo yanayoonyesha ni uchunguzi gani uliokuwa ukiendelea kati ya Desemba 2019, alipokamatwa, na Januari 2022, alipofikishwa mahakamani.

Nassor alidaiwa kukamatwa Desemba 3, 2019, katika eneo la Fuoni Kwa Mabala, Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar, akiwa na gramu 15.6211 za heroini.

Awali, Mahakama ya Mkoa ilimhukumu kifungo cha miaka saba baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na dawa hizo.

Hata hivyo, alipokata rufaa Mahakama Kuu, rufaa yake ilitupiliwa mbali na adhabu ikaongezwa kutoka miaka saba hadi 15 jela.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, askari wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya walimkamata wakati wa doria na, baada ya kumpekua, walidai walikuta mfuko mdogo wenye unga wa kahawia ambao baadaye Mkemia Mkuu wa Serikali alithibitisha kuwa ulikuwa heroini.

Nassor alikana madai hayo, akidai hakukamatwa akiwa na dawa za kulevya na kwamba, baada ya kukamatwa, aliachiwa kwa dhamana ya polisi na alitakiwa kuripoti kituoni kila siku huku akifanya kazi za usafi kwa muda mrefu kabla ya kufikishwa mahakamani zaidi ya miaka miwili baadaye.

Sababu za rufaa

Katika rufaa yake, Nassor aliwasilisha sababu nane akipinga hukumu na adhabu, akidai mahakama za chini zilikosea kumtia hatiani wakati upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka dhidi yake bila kuacha shaka ya msingi.

Pia alisema kuwa hakuwahi kukutwa na heroini na kwamba ushahidi uliotolewa dhidi yake haukuwa wa kuaminika wala wa kweli.

Kuhusu kuchelewa kufikishwa mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili bila sababu za msingi, alidai kulionyesha udhaifu wa kesi ya upande wa mashtaka na kulikiuka haki zake, hivyo akaiomba Mahakama ya Rufaa kufuta hukumu na kumuachia huru.

Upande wa mashtaka nao ulikiri kuwa haukuwa na maelezo yanayoonyesha kilichokuwa kinaendelea katika kipindi hicho, huku ukikubali kuwa uchunguzi wa dawa hizo ulikuwa umekamilika ndani ya siku chache baada ya kukamatwa kwake.


Uamuzi wa Mahakama

Jaji Mlacha amesema kuwa, ingawa kucheleweshwa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani si sababu ya moja kwa moja ya kufuta hukumu katika kila kesi, mazingira ya shauri hilo yalidhoofisha kwa kiasi kikubwa uaminifu wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mahakama imeeleza kuwa kama kweli mrufani angekamatwa akiwa na heroini kama ilivyodaiwa, isingekuwa na mantiki kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kumfungulia mashtaka, ilhali uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ulikuwa umekamilika ndani ya siku chache.

Majaji walibaini kuwa ucheleweshaji huo uliifanya hoja ya utetezi wa mrufani kuwa na uzito, hasa madai yake kwamba hakukamatwa akiwa na dawa za kulevya na kwamba aliendelea kuripoti kituoni kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani.

Mahakama pia ilisema Mahakama ya Mkoa na Mahakama Kuu zilishindwa kutathmini athari za ucheleweshaji huo katika uaminifu wa ushahidi wa mashahidi wa mashtaka.

Kutokana na mapungufu hayo, Mahakama ya Rufaa ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka dhidi ya Nassor bila kuacha shaka yoyote ya msingi. Hivyo, iliruhusu rufaa, ikafuta hukumu za Mahakama ya Mkoa na Mahakama Kuu pamoja na adhabu ya miaka 15 jela, na kuamuru Nassor aachiwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.