Aliyekuwa Mkurugenzi Iguwasa kizimbani kwa uhujumu uchumi

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imempandisha kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Igunga (Iguwasa), Hussein Nyemba (34) akikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Tabora. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imempandisha kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Igunga (Iguwasa), Hussein Nyemba (34) akikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka katika shauri la uhujumu uchumi namba 1/2023, Nyemba anadaiwa kupokea Sh4milioni kutoka kwa mfanyabiashara ili amlipe malipo yake aliyokuwa anaidai mamlaka hiyo.

Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani Aprili 25, 2023, ambapo Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Mazengo Joseph aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Igunga kuwa mshtakiwa Husseni Nyemba anadaiwa kutenda kosa hilo Julai, 2021.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Lydia Ilunda, mwendesha mashtaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo alipokuwa mtendaji mkuu wa Iguwasa kabla hajaamishiwa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.

“Mshtakiwa alijipatia manufaa kwa njia isiyo halali kinyume na Kifungu cha 23 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 329 mapitio ya 2019 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi,” Mwendesha Mashtaka huyo wa Takukuru ameieleza Mahakama

Mshtakiwa anadaiwa kujipatia kujipatia kiasi chicho ha Sh4 milioni kutoka kwa mfanyabiashara, Rashid Mwinyimkuu, mkazi wa Jiji la Dar es salaam aliyekuwa akidai malipo yake baada ya kutoa huduma ya vifaa kwa mamlaka ya Iguwasa.

Baada ya kusomewa mashtaka, Hussein Nyemba alikana mashtaka yake na shauri hilo kuahirishwa hadi Mei 16, 2023 ambapo mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali baada ya upande wa Jamhuri kuiambia Mahakama kuwa upelelezi umekamilika. Mshtakiwa ameachiwa kwa dhamana ya Sh2 milioni.