Aliyemkata koromeo mgambo, ahukumiwa kunyongwa
Mshtakiwa wa kesi ya mauaji Chesco Mveka akitoka katika ukumbi wa Mahakama kuu kanda ya Iringa ambayo imeketi wilayani Mufindi akielekea kupanda gari la Polisi baada ya kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa. Picha na Mary Sanyiwa, Mufindi
Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi Wilaya ya Mufindi, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa mkazi wa Kijiji cha Ugenza Wilaya ya Mufindi, Chesco Mveka (49) baada ya kukutwa na hatia ya kosa la mauaji ya Silayo Mbwimbije (35) ambaye alikuwa ni mgambo wa kijiji hicho kwa kukamta koromeo lake kwa kutumia kisu na kusababisha kifo chake.
Shauri hilo la mauaji namba 19/2016 ambalo lilikuwa na mashahidi wawili ambapo hukumu yake imetolewa Jumatano Machi 22, 2023 katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa ambayo imeketi wilayani hapa.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyoketi wilayani hapa, Ilvin Mgeta amesema kuwa mahakama imejiridhisha na ushaidi ambao ulitolewa kwa pande zote mbili wa mashtaka na utetezi na kumtia hatini mshtakiwa Chesco kwa kutenda kosa la mauaji.
Aidha Jaji huyo amesema mshtakiwa huyo amehukumiwa chini ya kifungu namba 196 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la mwaka 2022, ambapo adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa chini ya kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu rejeo 2016.
Hata hivyo Jaji huyo amesema kifungu hicho cha 197 kinatoa aina moja ya adhabu ambayo ni kunyongwa hadi kufa kwa mshtakiwa ambaye anapatika na hatia ya kosa kama hilo.
Adha Jaji huyo amedai kuwa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo umeonyesha mshtakiwa ambaye yupo mbele ya mahakama hiyo ndiye ametenda kosa hilo akiwa na nia ovu ya kusababisha kifo cha marehemu huyo.
"Kwa mazingira hayo inaonyesha wazi mshtakiwa aliyekuwa mbele ya mahakama hii, alitumia kisu kukata koromeo la marehemu hii inaonyesha mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kusababisha kifo kwa sababu baada ya kutenda kosa hilo alitoroka kijiji hapo hadi alipokuja kukamatwa 2016," ameeleza Jaji huyo.
Amesema kuwa katika shauri hilo linadaiwa kuwa mwanaume mtu mzima alimkata koo mwanaume mwengine ambaye ni muuaji. Hivyo kwa ukizingatia katika hali ya kawaida koo ni sehemu hatari ambayo ikizuliwa na kitu chenye ncha kali ni rahisi kusababisha mauti kwa mtu yoyote ambaye atashambulia kwenye maeneo hayo.
Pia akisoma maelezo hayo, Jaji Mgeta amesema kuwa inadaiwa kuwa Aprili 3, 2013 katika Kijiji cha Ugenza wilaya hapa, aliuawa mtu ambaye anaitwa Silayo Mbwimbije, ambapo mshtakiwa alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikana kutenda kosa hilo.
"Baada ya mshtakiwa kukana shtaka hilo upande wa mashta ukalazima kuleta mashahidi wawili kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma za mauaji hayo ambayo yalikuwa yanamkabili mshtakiwa huyo ambaye ni Chesco," amesema Jaji
Jaji Mgeta amefafanua kuwa mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo alidai kuwa siku ya tukio alikuwa shamba hadi muda wa saa saba mchana, lakini wakati anatoka shambani kwake alielekea moja kwa moja kwenye kilabu cha pombe kisha alirudi nyumbani kwake.
Mshtakiwa huyo alidai kuwa wakati akiwa njiani kurudi nyumbani kwake alikutana na kundi kubwa la watu njiani likimueleza kwamba Mbwimbije ameuawa mbele ya ofisi ya kata ya kijiji hicho.
Awali, akitoa maeleezo kabla ya hukumu hiyo mwendesha mashtaka wa Serikali Yahaya Misango ameiomba mahakama kuzingatia kifungu 197 kama kinavyoelekeza kuhusu mshtakiwa ambaye amepatika na hatia ya kosa kama hilo.
"Mahakama yako imemtia hatiani mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha kanuni ya adhabu ambayo ni kunyongwa hadi kufa hivyo ombi langu kwa Mahakama kujielekeza kwenye kifungu hicho," amesema Misango.
Kwa upande wa utetezi wakili Lazaro Hukumu amesema baada ya mteja wake kukutwa na hatia hakuwa na ombi kwa mahakama kwa kuzingatia kosa hilo halina adhabu mbadala.