Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyemlawiti mtoto wa rafiki yake akwama Mahakama Kuu

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imetupilia mbali rufaa ya Frank Joseph aliyekuwa akipinga hukumu ya kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kike wa rafiki yake mwenye umri wa miaka 11.

Geita. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imebariki hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya mkazi wa Geita, Frank Joseph, aliyepatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kike wa rafiki yake mwenye umri wa miaka 11.

Uamuzi huo ulitolewa Mei 18, 2026 na Jaji Griffin Mwakapeje baada ya kutupilia mbali rufaa ya Joseph aliyekuwa akipinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Geita iliyotolewa Februari 16, 2026.

Katika hukumu yake, Jaji Mwakapeje amesema mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha uliothibitisha bila kuacha shaka kuwa Joseph alitenda kosa hilo Agosti 21, 2025 katika eneo la Balenge mkoani Geita.

Joseph alikuwa ameshtakiwa kwa kosa moja la ulawiti kinyume na kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, huku upande wa mashtaka ukiwasilisha mashahidi 10.


Ushahidi wa upande wa mashtaka

Mahakamani ilidaiwa kuwa siku ya tukio mtoto huyo alikuwa amelala chumbani pamoja na dada yake, huku mlango wa chumba ukiwa haujafungwa.

Katika ushahidi wake, mtoto huyo alidai alishtuka na kumwona Joseph, ambaye ni rafiki wa baba yake, akiwa ndani ya chumba hicho huku taa ikiwa imewashwa.

Alidai kuwa alijikuta akiwa uchi, ambapo mtuhumiwa alimziba mdomo, akamtishia na kisha kumbaka. Mtoto huyo alieleza kuwa alipata maumivu makali na kumuomba mtuhumiwa amruhusu kwenda kujisaidia.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, wakati mtuhumiwa akiendelea na kitendo hicho, alijaribu pia kumvua nguo mtoto mwingine aliyekuwa amelala chumbani humo.

Baada ya kupewa nafasi ya kutoka kwenda kujisaidia, mtoto huyo alimfungia mtuhumiwa chumbani kwa nje na kukimbilia kutoa taarifa kwa watu waliokuwa jirani.

Shahidi wa saba alidai kuamshwa na mtoto huyo aliyemweleza kuwa kuna mtu ameingia chumbani na kumlawiti. Shahidi huyo alisema alimfungia mtuhumiwa kwa kufuli ndani ya chumba hicho kabla ya kutoa taarifa kwa mama wa mtoto na baadaye polisi.

Kwa upande wake, shahidi wa nane ambaye ni mgambo, alisema alipofika eneo la tukio alikuta watu wamekusanyika.

Alieleza kuwa baada ya kufungua chumba kilichokuwa kimefungwa kwa nje, alimkuta Joseph akiwa amelala kitandani bila suruali na ndipo alipokamatwa.

Daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo alieleza mahakamani kuwa uchunguzi wa kitabibu ulionyesha dalili za kupenya kwa kitu butu pamoja na michubuko na kulegea kwa misuli katika sehemu za siri.

Alisema mtoto huyo alipatiwa dawa za kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa na Virusi vya Ukimwi.

Aidha, shahidi aliyerekodi maelezo ya onyo ya Joseph alisema mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo katika maelezo yake.


Utetezi wa Joseph

Kwenye utetezi wake, Joseph alidai kesi hiyo ilitengenezwa kutokana na mgogoro wa deni la Sh400,000 kati yake na familia ya mtoto huyo.

Alidai kuwa alikamatwa alipokwenda kudai fedha hizo na kwamba alilazimishwa kukiri kosa hilo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika rufaa yake, aliomba Mahakama Kuu ibatilishe hukumu hiyo akidai ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu, wenye utata na wenye mapungufu ya kisheria.


Mahakama ilivyotupilia mbali rufaa

Akitoa uamuzi, Jaji Mwakapeje alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi mbalimbali uliunga mkono simulizi ya mtoto huyo na kuthibitisha uwepo wa Joseph eneo la tukio muda mfupi baada ya tukio kutokea.

Mahakama ilisema ushahidi huo uliondoa uwezekano wowote wa kutambua mtu mwingine kimakosa.

“Mrufani hakutambuliwa tu kwa sababu alikuwa akifahamika kwa familia ya mtoto, bali pia alikamatwa ndani ya chumba hicho muda mfupi baada ya tukio kutokea,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Mahakama pia ilizingatia ushahidi wa kitabibu uliowasilishwa na daktari aliyemchunguza mtoto huyo.

Jaji Mwakapeje alisema Joseph hakuwahi kupinga maelezo yake ya onyo wakati yalipowasilishwa mahakamani kama ushahidi, hivyo hakuwa na msingi wa kuibua hoja hiyo kwa mara ya kwanza katika hatua ya rufaa.

Mahakama ilieleza kuwa hata kama maelezo hayo yasingezingatiwa, bado ushahidi mwingine uliowasilishwa ulikuwa wa kutosha kuthibitisha kosa hilo.

Pia, mahakama ilikataa madai ya Joseph kuwa kesi hiyo ilichochewa na mgogoro wa deni la Sh400,000, ikisema hakuwasilisha ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo wala kuwauliza mashahidi kuhusu suala hilo wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, maelezo ya Joseph kwamba alifika nyumbani hapo kudai deni hayakuweza kueleza sababu ya kukutwa ndani ya chumba cha mtoto akiwa hana suruali.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha vipengele vyote vya kosa hilo bila kuacha shaka yoyote na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.