Prime
Aliyemuua mtoto kisa mchele ahukumiwa kunyongwa
Muktasari:
- Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Bukoba imemhukumu adhabu ya kifo Ravisi Mshobozi, baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya mtoto Mjuni Mathias kwa kumkata kwa panga.
Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Tanzania ya Bukoba imemhukumu Ravisi Mshobozi, mkazi wa Kijiji cha Rukindo, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto Mjuni Mathias kwa kumkata kwa panga.
Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 21, 2026, na Jaji Immaculata Banzi, aliyesema upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka yoyote kuwa mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha mtoto huyo kwa makusudi.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, tukio hilo lilitokea Oktoba 10, 2024, asubuhi katika kijiji hicho, na mshtakiwa alifika nyumbani kwa baba wa marehemu, Mathias Mathayo (shahidi wa kwanza), akiwa na panga na kuomba sehemu ya kunoa.
Baada ya kunoa panga, alidaiwa kuomba magimbi, ambapo mtoto huyo (marehemu kwa sasa) alienda kumng’olea shambani.
Baadaye, aliwashawishi marehemu na watoto wenzake kwenda nyumbani kwake akiahidi kuwapa mchele badala ya magimbi.
Hata hivyo, ushahidi wa shahidi wa pili, ambaye alikuwa mtoto, ulieleza kuwa walipofika nyumbani kwa mshtakiwa, aliwakaribisha na kupima mchele, lakini ghafla aliwashika mikono.
Wakati yeye na mwenzake walipofanikiwa kukimbia, marehemu alibaki mikononi mwa mshtakiwa.
Katika hukumu yake, Jaji huyo amesema kuwa, baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa kesi hiyo ilithibitishwa bila kuacha shaka.
Ushahidi
Shahidi wa pili alidai mahakamani kuwa alishuhudia kwa macho yake mshtakiwa akimkata marehemu kichwani na miguuni kwa panga, hali iliyosababisha aanguke chini.
Baada ya tukio hilo, alikimbia nyumbani na kumweleza baba yake, aliyefika eneo la tukio na kumkuta mwanawe akiwa amefariki dunia mbele ya nyumba ya mshtakiwa, akiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, shingoni na miguuni.
Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alijifungia ndani ya nyumba yake baada ya tukio, lakini alipotoka, alikimbia akiwa na panga, huku wananchi wakimfukuza.
Shahidi wa tano, Julius Manziwa, alithibitisha kumuona mshtakiwa akikimbia na panga mkononi, huku akifukuzwa na baba wa marehemu na wananchi wengine.
Mshtakiwa alikimbilia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Charles Tibendelana (shahidi wa saba), na kujifungia ndani, na baadaye alikamatwa na polisi akiwa bado ameshikilia panga iliyodaiwa kutumika kutekeleza mauaji hayo.
Polisi walieleza kuwa panga hiyo ilikuwa na damu na ilipokelewa kama kielelezo mahakamani.
Shahidi wa tatu, Dk Ivan Kandubuka, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alieleza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali, ikiwemo kichwani, shingoni, mkononi na mguuni.
Alibainisha kuwa kifo kilitokana na upotevu mkubwa wa damu uliosababisha ubongo kukosa oksijeni.
Katika ushahidi mwingine muhimu, polisi waliwasilisha maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ambayo yalionesha kuwa alikiri kutekeleza mauaji hayo, ingawa mshtakiwa alipinga uhalali wa taarifa hiyo, akidai alilazimishwa kuisaini. Mahakama ilikataa hoja hiyo baada ya kufanya uchunguzi maalumu.
Utetezi
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana kuhusika na mauaji hayo na kudai siku ya tukio alikuwa akisafisha shamba kwa ajili ya kupanda mahindi, na kusikia kelele na alipofika nyumbani kwake alikuta watu wengi wamekusanyika wakiwa na panga.
Alidai baada ya kumuona, watu hao walimkaribia kwa lengo la kumkamata, na alipohisi hatari, alikimbia kuelekea katikati, ila kabla hajafika walimkamata, wakimtuhumu kuhusika na mauaji hayo.
Aliieleza mahakama kuwa walianza kumshambulia na kumpeleka nyumbani kwa mwenyekiti na kumfungia ndani.
Aidha, alikana kwenda kuchukua viazi vikuu kwa shahidi wa kwanza, kumiliki panga lililodaiwa kuhusika kwenye mauaji hayo, na kuwa alisaini hati ya ukamataji baada ya kulazimishwa na kupigwa kwa kutumia rungu, na kuomba mahakama imwachie huru.
Uamuzi wa Jaji
Mahakama ilieleza ushahidi wa mashahidi pamoja na mazingira ya tukio uliunga mkono maelezo yaliyomo katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo.
Hata hivyo, Jaji Banzi amesema utetezi huo haukuwa na mashiko, kwani haukuungwa mkono na ushahidi wowote na ulipingana na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Mahakama ilisisitiza kuwa katika kesi za jinai, mzigo wa kuthibitisha kosa uko kwa upande wa mashtaka, lakini katika kesi hiyo ushahidi uliwasilishwa kwa uzito wa kutosha kuthibitisha hatia ya mshtakiwa.
Jaji Banzi alibainisha kuwa vipengele vyote vinavyounda kosa la mauaji vilithibitishwa, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa kifo, sababu ya kifo kuwa si ya kawaida, uhusiano wa mshtakiwa na tukio, pamoja na uwepo wa nia mbaya.
Alieleza kuwa aina ya silaha iliyotumika, sehemu za mwili zilizolengwa na idadi ya majeraha ni ushahidi tosha wa kuonyesha nia ya kuua.
“Kwa kuzingatia ushahidi wa moja kwa moja na wa mazingira, pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa, mahakama inaridhika kuwa mshtakiwa ndiye aliyemuua marehemu kwa nia ya makusudi,” amesema Jaji Banzi.
Kutokana na uamuzi huo, mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.