Aliyewapatanisha Rais Kenyatta na Odinga atua tena Kenya

Muktasari:
- Seneta wa jimbo la Delaware nchini Marekani, Chris Coons ambaye pia alihusika kwenye maridhiano ya Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa mshindani wake wa karibu kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2017, Raila Odinga amefika nchini Kenya.
Dar es Salaam. Seneta wa jimbo la Delaware nchini Marekani, Chris Coons ambaye pia alihusika kwenye maridhiano ya Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa mshindani wake wa karibu kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2017, Raila Odinga amefika nchini Kenya.
Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter ya balozi wa Marekani nchini Kenya, Margaret Whitman imeonyesha kuwa mwanadiplomasia huyo amewasili leo Alhamisi Agosti 18, 2022 saa 6.25 usiku.
“Najisikia vizuri kumkaribisha Chris Coons na ujumbe wake alioongozana nao, huku Kenya ikiwa kituo cha tatu cha ziara yao kati ya nchi tano za Afrika,” ameandika Balozi Whitman kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Seneta huyo wa jimbo la Delaware mwaka 2018 alifanikisha kufanyika kwa maridhiano ya kisiasa kati ya Kenyatta na Odinga ambaye alisema mzozo huo ungesababisha athari hasi kwa nchi ya Kenya.
“Mzozo wa kisiasa wa Kenya ungeweza kuwa mbaya zaidi ikiwa usingeshughulikiwa kwa haraka,” moja kauli ya Coons kuhusu usuluhishi alioufanya mwaka 2018.
Coons amefika nchini Kenya ikiwa ni siku moja tangu mgombea urais wa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga na viongozi wa muungano huo wakubaliane kwenda kuyapinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani.
Hata hivyo, Whitman amesema kuwa Coons na ujumber wake kwenye ziara yao watakutana na watoa huduma za afya na mashirika yanayowawezesha wasichana nchini humo.