Amuua dereva bajaji kisha kumfukia shimoni akimtuhumu kutembea na mkewe

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao akionesha baadhi ya vipande vya bomba vilivyokamatwa. 

Muktasari:

Mwanaume mmoja (jina limehifadhiwa) anatuhumiwa kumuua kisha kumfukia kwenye shimo dereva bajaji, Benedicto Modest (40) kwa kudhani anamahusiano ya kimapenzi na mke wake.

Tabora. Mkazi wa Kitongoji cha Utusini Kata ya Misha mkoani Tabora, Benedicto Modest (40) ameuawa kisha mwili wake kufukiwa kwenye shimo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema Benedicto ambaye alikuwa dereva bajaji alipigwa na kitu kizito kichwani na kisha kufukiwa kwenye shimo na msaidizi wake aliyekuwa akishirikiana naye kwenye kazi hiyo.

Amesema chanzo cha mauaji hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita ni wivu wa mapenzi akidai mtuhumiwa alikuwa anamuhisi mwenzake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake.

Abwao amesema msaidizi huyo aliwahi kumuonya bosi wake mara kadhaa pasipo mafanikio na ndipo alipoamua kujichukulia sheria mkononi kwa kumuua na kisha kumfukia shimoni.

“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwaajili ya uchunguzi,”amesema

Abwao amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo atafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo linawashikilia watu 21 mkoani humo kwa tuhuma za kuiba miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tabora (Tuwasa).

Abwao amesema watu hao wamekamatwa kutokana na msako unaofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na watumishi wa Tuwasa, halmashauri na vyombo vingine vya usalama.

Amesema watuhumiwa hao pia wamekutwa na mali mbalimbali za wizi vikiwemo vifaa kwa ajili ya upatikanaji wa maji ambavyo ni  koki 43, gatevalve 11, stendi za mita za maji, vipande vya bomba 21, bomba 33, nondo 353, bati tatu, vipande vya bomba za barabarani 12 na vitanda vya chuma vya majokofu ya chumba cha kuhifadhia maiti viwili.

“Haya ni mafanikio makubwa tumepata katika msako unaoendelea hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Idd,”amesema

Abwao amesema kumekuwa na malalamiko ya wananchi kulalamikia kuibiwa miundombinu ya maji na ndio maana msako huo umepata mafanikio ya kuwabaini baadhi ya  watuhumiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tuwasa, Mayunga Kashilimu amesema kumekuwa na wimbi la wizi wa baadhi ya vifaa vya miundombinu ya maji na wateja wao kulalamika huku wakiipa hasara mamlaka yake.

Amesema wanalenga kutoa huduma bora kwa wateja wao lakini wizi wa miundombinu unaweza kukwamisha jitihada zao za kuwahudumia kwa ubora nakudai hawatakata tamaa na kukwamishwa na baadhi ya wahujumu wa miundombinu ya maji.