Anusurika kifo baada ya kuangukiwa na ukuta

Askari akionyesha eneo ukuta wa ghorofa ulipodondoka
Muktasari:
- Mtu huyo ameangukiwa na ukuta katika jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa mkoani Morogoro. Alikimbizwa hospitali muda mfupi baada ya kunusurika kupoteza maisha katika ajali hiyo.
Morogoro. Mtu mmoja mkazi wa kata ya Mwembesongo, manispaa ya Morogoro, Ibrahim Ramadhani (44) amenusurika kifo baada ya kuangukiwa na ukuta wa jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa katika Mtaa wa Sugume, mkoani Morogoro.
Hata hivyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo limefanya jitihada za kumuokoa mtu huyo ambapo baada ya kuokolewa amepekekwa hospitali ya rufaa ya mkoa kwa matibabu zaidi.
Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 3, 2024, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro, Ramadhan Marugujo amethibitisha kumuokoa Ramadhan (44) aliyepata ajali ya kuangukiwa na ukuta.
Marugujo amesema: “Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tulipata taarifa za uwepo wa ajali ya mtu kuangukiwa na ukuta, haraka tulifika hapa na tukamkuta amebanwa sehemu ya miguu kuanzia kiunoni. Jitihada za kuuondoa ule ukuta uliokua umemkandamiza zilifanyika na baadae tukampeleka hospitali ya rufaa ya mkoa kwa ajili ya matibabu zaidi.”
“Tulichogundua kwa haraka hapa ni ujenzi wa ghorofa hili haukuzingatia vipimo halisi maana aliyepata ajali alipewa kazi ya kuondoa mbao zilizokuwa juu ya ghorofa huku wenzake wakiwa wanazitoa kwenye moja ya maeneo ambayo ujenzi ulikua unaendelea na kwa kua Ibrahim alikua chini kabisa, ndipo ukuta ukamuangukia na kumbana sehemu za miguu yake.”
Hata hivyo, Kamanda Ramadhan amewaomba wanaoendesha shughuli za ujenzi katika manispaa na mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanafuata vipimo vya ujenzi kwani uchunguzi wa awali umeonyesha ujenzi wa ghorofa lile haukuzingatia vipimo.
“Tumejaribu kuchunguza tumeona hata nondo zilizokuwa zimetumika kujengea baadhi ya nguzo zilikuwa zimechanganywa maana kuna nondo za milimita 16 na zile za milimita 24 zilikua zimechanganywa na hata resho ya saruji ilikuwa ndogo kiasi kwamba ule ukuta ungeanguka wakati wote, hivyo natoa wito kwa wajenzi kufuata miiko ya ujenzi, waache kujenga ilimradi tu,” amesema.
Shuhuda wa tukio hilo, Benson Emmanuel amesema alikua anakunywa supu kabla ya kusikia kishindo cha jkuta huo ukindondoka
“Nilikuwa nakunywa supu jirani na eneo hili, wakati naendelea nikasikia kishindo, kugeuka nikaona ukuta umeanguka na baada ya muda nikaona watu wamejazana na mi mimi nikasogwa ndipo nikakuta mwenzetu amebanwa na ukuta sehemu ya miguu,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Kwa nilivyoona alikua na hali mbaya maana tumetumia kama nusu saa hivi kumuokoa na kwa nilivyomuona alikua ameumia sehemu ya miguu na kwa maoni yangu ule ukuta umedondoka kutokana na mvua kubwa ambazo zimenyesha,” amesema.
Kwa upande, Salvator Medadi aliyekuwa akipita njia wakati wa ajali hiyo, amesema alianza kuona udongo unadondoka taratibu kuanzia chini na aliyepata ajali hiyo alikua amekaa pembeni mwa ukuta huo, alipojaribu kutoka eneo hilo, ukuta ukamwangukia.