Asilimia 41 ya maji yaliyopimwa mwaka 2023 hayana viwango

Muktasari:

  • Sampuli 6,490 za maji zilikusanywa na kuhakikiwa ubora katika mwaka 2023 ikilinganishwa na sampuli 6,344 zilizohakikiwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 2.3.

Dar es Salaam. Asilimia 41.6 ya sampuli 5,764 za maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani zilizofanyiwa vipimo mwaka 2023 zilikuwa hazikidhi viwango vya ubora na usalama wa maji vinavyokubalika kimataifa.

Hayo yamebainishwa kupitia Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kilichotolewa leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa, katika mwaka 2023 matokeo ya uhakiki wa ubora wa maji katika sampuli 5,764 za matumizi ya majumbani yalionesha kuwa sampuli za maji 3,365 pekee ndiyo zilikidhi viwango vya ubora na usalama wa maji vinavyokubalika kimataifa.

“Sampuli 2,399 hazikukidhi viwango. Kutokidhi viwango kwa sampuli hizo kulitokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha rangi, tope, ugumu wa maji, madini ya chumvi, nitrate, fluoride, manganese na chuma katika maeneo mbalimbali nchini,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia uwepo kwa vimelea vya vijidudu katika skimu za usambazaji maji zisizokuwa na miundombinu ya kutibu maji pamoja na uwepo wa kiasi kidogo cha dawa ya chlorine baki katika skimu za usambazaji maji zenye miundombinu ya kutibu maji kulichangia kutofikiwa kwa viwango vya ubora na usalama wa maji unaotakiwa.

Sampuli hizo ni kati ya zile sampuli 6,490 za maji zilizokusanywa na kuhakikiwa ubora katika mwaka 2023. Sampunli zilizochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi ni ongezeko la asilimia 2.3 ikilinganishwa na zilizochunguzwa mwaka uliotangulia.

Ongezeko hilo linatajwa kuchangiwa na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi wa ubora wa maji katika maabara za Mtwara, Singida, Morogoro na Tanga pamoja na matengenezo yaliyofanyika kwenye vifaa vya uchunguzi wa ubora wa maji katika maabara ya Dar es Salaam.

“Mbali na sampuli za maji yanayotumika majumbani pia sampuli 233 zilikuwa za ufuatiliaji wa mwenendo wa ubora wa maji katika vyanzo vya maji, sampuli 71 za utafiti, sampuli 242 matumizi ya viwandani, 24 katika umwagiliaji, 49 ujenzi na sampuli 107 kupima uwezo wa utendaji kazi wa maabara,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Imeelezwa kuwa, sampuli zote 315 za maji kwa ajili ya shughuli za viwandani, umwagiliaji, ujenzi, utafiti na upimaji wa uwezo wa utendaji kazi wa maabara zilifanyiwa uhakiki na kukidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kwa matumizi husika.

Pia matokeo ya uhakiki wa sampuli 233 kutoka vyanzo vya maji yalionesha kuwa havikuathiriwa na hali ya miamba ya asili, shughuli za kibinadamu, jiografia ya eneo na mabadiliko ya tabianchi na hivyo, kuwa rafiki kwa mazingira na viumbe hai vilivyomo.

Kwa upande mwingine, sampuli 377 za majitaka yanayorudishwa kwenye mazingira zilikusanywa na kuhakikiwa ubora ikilinganishwa na sampuli 446 zilizohakikiwa ubora mwaka 2022.

Matokeo ya uhakiki yalionesha kuwa sampuli 122 sawa na asilimia 32.4 hazikukidhi viwango vya ubora kutokana na kuwepo kwa Chemical Oxygen Demand (COD), Biological Oxygen Demand (BOD), Nitrate na Phosphate kuliko kiwango kinachohitajika kwa ajili ya maji hayo kurudishwa kwenye mazingira.