Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asilimia 68 ya wanufaika wa Tasaf Mbeya wanatumia bima ya afya kwa wote

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mbeya, Dk Eliud Kilimba, akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake kuhusu mwenendo wa zoezi la kuandikisha makundi maalumu katika mpango wa bima ya afya kwa wote. Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Takribani watu 30,000 kutoka kaya 7,000 katika halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya wanatarajiwa kunufaika na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote baada ya kulipiwa gharama na Serikali.

Mbeya. Asilimia 68 ya wananchi kutoka makundi maalumu katika halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya, wameingizwa kwenye Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote tangu Februari 2026 baada ya Serikali kuuzindua rasmi.

Idadi hiyo inahusisha watu 30,000 kutoka kaya 7,000 zilizotambuliwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) ambao gharama zao za bima zimelipiwa na Serikali ili kuhakikisha makundi yasiyojiweza yanapata huduma za afya kwa urahisi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Juni 27, 2026, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mbeya, Dk Eliud Kilimba amesema usajili unaendelea sambamba na ugawaji wa kadi za bima kwa walengwa ili waanze kupata huduma katika vituo vya afya vilivyosajiliwa.

“Walengwa watapata huduma katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa, rufaa za kanda na taifa, hospitali binafsi na taasisi za kidini zilizosajiliwa na NHIF,” amesema.

Amesema kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali imesajili zaidi ya vituo 10,000 vya kutolea huduma za afya nchini, hatua itakayowawezesha wanachama kupata matibabu katika eneo lolote walipo.

Dk Kilimba amesema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kupitia mfumo huo, hususan makundi ya wanufaika wa Tasaf katika awamu ya kwanza ya majaribio.

“Utekelezaji ulianza Februari mwaka huu baada ya waziri mwenye dhamana kuzindua mpango huo kuanzia makundi maalumu yanayolipiwa na Serikali, hususan kaya zisizojiweza kupitia mpango wa Tasaf,” amesema.

Amesema Mkoa wa Mbeya ulipangiwa kuandikisha watu 30,000 kutoka kaya 7,000, na hadi sasa umefikia asilimia 68 ya walengwa huku kila kaya ikitarajiwa kunufaisha watu sita kupitia bima hiyo.


Changamoto za walengwa

Dk Kilimba amesema changamoto zinazokwamisha kufikiwa kwa lengo la asilimia 100 ni baadhi ya walengwa kuhama makazi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na wengine kutopatikana kutokana na kukosa mawasiliano.

“NHIF tumejipanga kufikia malengo kwa kuendelea kutoa elimu katika vijiji, vitongoji na kata, sambamba na kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa dini na viongozi wa kimila kuhamasisha wananchi,” amesema.

Amesema utambuzi wa walengwa kupitia Tasaf umerahisisha zoezi hilo kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa kuwafikia katika maeneo yao.

Kuhusu makundi mengine kujiunga na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Dk Kilimba amesema NHIF inasubiri tamko la Waziri mwenye dhamana kabla ya kufungua usajili kwa wananchi wengine.

“Tunawashauri wadau kama vile waandishi wa habari, waendesha bodaboda, wakulima na makundi mengine kujiandaa kujiunga mara dirisha litakapofunguliwa kwa gharama ya Sh150,000,” amesema.

Hata hivyo, amesema mwitikio wa makundi maalumu kujiunga na bima ya afya kwa hiari bado ni mdogo kutokana na wananchi wengi kujikita katika shughuli za kiuchumi, licha ya jitihada za Serikali kuendelea kutoa elimu.


Maoni ya wananchi

Mkazi wa Nonde, Rehema Mwanjonde amesema Serikali inapaswa kufanya uhakiki zaidi ili kuwabaini wananchi wenye uhitaji mkubwa wa bima ya afya kutokana na changamoto za kiuchumi.

“Bado wapo wananchi wengi wenye uhitaji mkubwa kutokana na hali duni ya kiuchumi. Ni muhimu nao wapate fursa ya kunufaika na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote,” amesema.

Naye, dereva wa bajaji, Peter Fredy, amesema Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa makundi mengine wakati ikiendelea kukamilisha usajili wa walengwa wa awamu ya kwanza ili kuongeza uelewa na maandalizi kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa kwa wananchi wote.