Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asimulia alivyopewa adhabu kwa saa mbili hadi ujauzito kuharibika

Asimulia alivyopewa adhabu kwa saa mbili hadi ujauzito kuharibika

Muktasari:

  • Asha Rajabu(28) mkazi wa kijiji cha Samanga Marangu wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amesimulia namna alivyorukishwa kichurachura na mwenyekiti wa kijiji hicho, kwa madai ya kuchelewa kufunga baa na kusababisha ujauzito wake wa miezi miwili kuharibika.

Moshi. Asha Rajabu(28) mkazi wa kijiji cha Samanga Marangu wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amesimulia namna alivyorukishwa kichurachura na mwenyekiti wa kijiji hicho, kwa madai ya kuchelewa kufunga baa na kusababisha ujauzito wake wa miezi miwili kuharibika.

Mwenyekiti huyo, Wilfredy Minja kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, kwa tuhuma ya kumsababishia Asha mateso na kupoteza ujauzito.

Akizungumza na gazeti hili, Asha alieleza kuwa kwa zaidi ya miaka mitano, amekuwa akisumbuka kutafuta ujauzito bila mafanikio mpaka hapo alipobahatika kuupata ujauzito huo, lakini baada ya kupata masaibu hayo, furaha yake imemtumbukia nyongo.

“Ilikuwa ni Januari 24 mwaka huu, majira ya saa sita na nusu ambapo tunafunga baa muda huo, lakini wakati tunafunga walikuja wateja wawili wanahitaji chakula, nikamwambia mlinzi wafungulie tu tuwapikie,”

“Mimi nakaa hapo hapo kwa ndani, basi nikamwambia yule binti anayehusika na mambo ya jikoni awaandalie. Chakula kiliiva saa saba kamili maana huwa tunapika kwa oda, baada ya chakula kuiva wakasema hawawezi kula muda umeenda, lakini muda huo walikuwa na kiredio chao cha mkononi wakawa wanasikiliza muziki kwa kupitia hicho kiredio, baada ya kuwafungia chakula wakawa wanaondoka nikamwambia mlinzi wafungulie waondoke,”

Kilichofuatia baada ya wateja wale kuondoka, Aisha alisema kuwa kwa nje kulikuwa na sungusungu wakawaambia wabaki ndani na wateja wao.

Aliendelea kusema; ‘‘Basi nikiwa ndani nikasikia nje kuna kelele ikabidi nitoke nijue kuna shida gani. Nikawaambia naomba mnisamehe kwa kuchelewa kufunga, wakanambia kuna faini ambayo napaswa kulipa kwa kuchelewa kufunga. Nikawaambia ni shilingi ngapi wakaniambia ni Sh50,000, Nikawaambia sawa natoa hiyo fedha, ili wateja wangu waende, nikawaambia sitarudia kuchelewa kufunga tena,”

“Sasa wakati huyo mwenyekiti alikuwa bado hajafika ikabidi tumsubiri mpaka saa nane usiku, mwenyekiti alipofika akauliza wale sungusungu meneja hapa ni nani wakamwambia ni yule dada pale. Akanambia sogea mpaka hapa nilipo nikamfuata,akanambia wewe ndio umechelewa kufunga baa nikamweleza kuwa baa ilishafungwa ni wateja waliokuja kuchukua chakula,” alieleza Asha.

Baada ya hapo Asha alisema kuwa mwenyekiti huyo akamwamuru kuruka kichura. Pamoja na kumuomba kuwa hatoweza kufanya hilo kwa sababu ya kusikia maumivu, Asha alidai kuwa mwenyekiti hakutaka kumsikia na badala yake alianza kumpiga fimbo za kwenye makalio na mapaja.

Alisema kuwa adhabu ilianza saa nane usiku na iliendelea hadi saa kumi alfajiri. Licha ya kumuomba sana amwachie, alidai kuwa mwenyekiti aliendelea kumwadhibu kwa fimbo.

“Baada ya kumaliza kunipigisha kichura na vichapo akanambia nipige magoti, wale wenzangu waliokuwa ndani akaamuru nao watoke ili wapate adhabu kama mimi nilivyopata adhabu ile. Waliogopa ile adhabu wakataka kukimbia mwenyekiti sasa ndipo alipotoa bastola yake aliyokuwa nayo na kuwaambia mtu yeyote atakayekimbia nitamvunja mguu ikabidi watii baada ya kuona ile silaha nao wakaanza kuruka kichura kwa adhabu ile ile niliyopata,”alisema.

Aliendelea “Saa kumi na mbili asubuhi ilipofika akasema anataka faini yake ya Sh300,000 nikamwambia sina mwenyekiti, akanambia hapana na wakati huo nilikuwa na maumivu makali sana. Nikamuomba nikimwambia sina hiyo hela nina Sh200,000 akanambia hapana, kwa sababu nilikuwa na maumivu makali sana ya tumbo ikabidi nikubali nitoe ile hela,”

“Sasa baada ya hapo tumbo lilizidi kuniuma nikawaza nitafanyaje kwa sababu nilichelewa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi basi nilishindwa cha kufanya,’’alieleza.

Asha alisema kuwa Februari 4 akalazimika kwenda kituoni na kupewa PF3 na kisha kwenda hospitali alipofanyiwa vipimo na kubainika kuwa ujauzito ulitoka hivyo akatakiwa kusafishwa.

‘‘Hapa bado naendelea na matibabu maana bado nasikia maumivu,”alisema binti huyo

Aliongeza; ‘‘Kwa kweli alinifanyia tukio la kinyama maana huu ujauzito mpaka nimeupata niliutafuta kwa zaidi ya miaka mitano, kwa kweli nimeumia sana na sina cha kusema namkabidhi Mungu kwa sababu sijaona kosa kubwa la kuadhibiwa kiasi hicho, namwachia Mungu.’’

Kwa mujibu wa taarifa ya hospitali aliyotibiwa Asha, ni kweli kuwa binti huyo alikuwa na ujauzito wa miezi miwili uliotoka na hivyo kulazimika kusafishwa.Mpaka sasa mwenyekiti wa kijiji hicho anashikiliwa na Jeshi la Polisi, huku Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona akisema mwenyekiti huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kwa kutenda kosa hilo.