Askofu ataka uhuru wa habari ulindwe

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Askofu Emaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Morovian, amesema vyombo vya habari na jicho la umma hivyo uhuru wake ulindwe.
Amesema Serikali haipaswi kuweka mazingira kuminya vyombo vya habari na uhuru wa habari kwani kwa kufanya hivyo mambo mengi yatakuwa yanakwenda hovyo
Askofu Mwamakula ameyasema hayo jana Januari 20 katika mkutano wa wanahabari ulioandaliwa na Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) jijini hapa.
“Vyombo vya habari vikiwa huru vyama vya siasa haviwezi kufanya mambo ya hovyo, chama tawala, Serikali, makundi na vyama vingine vitaogopa kufanya hovyo hivyo Taifa litapiga hatua za kimaendeleo” alisema.
Askofu Mwamakula baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 walioshinda walitunga sheria, kanuni na kuweka taratibu za kuminya uhuru wa habari kwa sababu wanazozijua wenyewe.
“Nguvu, fedha na njia zisizofaa zilitumika kuminya vyombo vya habari, vilikabwa na matokeo yake vipo vilivyokufa, kuzimia, mahututi na vilisalimika viliogopa kuandika ukweli,” amesema
Askofu Mwamakula amesema hata hivi sasa ameanza kuona ukombozi unakuja baada ya kuwepo kwa harakati mbalimbali wa kurekebisha sheria zinazolalamikiwa kukandamiza uhuru wa habari na maeneo mengine.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, amesema wanaamini safari ndefu ya kutaka marekebisho kwenye Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 itafikia mwisho wakati Serikali itakapowasilishwa bungeni muswada huo.
Balile amesema wanaamini hivyo kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliwaahidi alipokutana na wadau wa tasnia ya habari.
Asema vyombo vya habari na waandishi havipaswi kuminywa kwa kuwa husaidia kuchochea maendeleo na kufichua mambo yanapokwenda isivyotakiwa.
“Tunaamini mwezi ujao mabadiliko hayo yatakuwa yamefanyika na taratibu mbalimbali za kutunga kanuni na uundaji wa vyombo vinavyotakiwa vitaanza ikiwemo utungaji wa kanuni na uanzishwaji wa vyombo vya kusimamia wanahabari” alisema
Amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani kumekuwa na mwelekeo mzuri na ushirikiano kati ya wadau sekta ya habari na Serikali.
Naye Mwandishi wa Simon Patrick, amesema anaamini mjadala wa marekebisho ya Sheria za habari utafanyika kwa kuzingatia masilahi ya Taifa na si vyama au kuangalia kundi fulani la watu.
“Tunaathirika sana na uamuzi wa chama tawala na Serikali yake vinataka nini, lakini naamini kilichotokea mwaka 2016 hakitajirudia na tutapata sheria nzuri” alisema
Mwandishi wa gazeti la Citizen Beatrice Materu, alisema uhuru wa habari hukuza demokrasia na sekta mbalimbali hivyo ni vema mambo yote yanayolalamikiwa yakaondolewa.