Askofu Gwajima aitahadharisha Serikali kuhusu chanjo za corona

Askofu Gwajima aitahadharisha Serikali kuhusu chanjo za corona

Muktasari:

  • Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima ameshauri Serikali kuwa makini na madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi iwapo Taifa litaruhusu chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona kutumika nchini.

Dodoma. Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima ameshauri Serikali kuwa makini na madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi iwapo Taifa litaruhusu chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona kutumika nchini.

Gwajima ameyasema hayo leo Jumanne Mei 11,  2021 wakati akichangiwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwaka 2021/22.

Amesema hayuko kinyume na chanjo bali yuko makini na aina ya chanjo za ugonjwa huo.

Huku akitaja aina tatu za chanjo ya ugonjwa huo, amebainisha kuwa ni tofauti na chanjo nyingine zilizokuja duniani ambazo zilikuwa zikichukua kati ya miaka nane hadi 10 kabla ya kuanza kutumiwa.

“Ni chanjo za mwendo kasi unapojaribu kuuliza kwa nini inakuwa haraka wanasema sababu ni kukuwa kwa teknolojia, wamemobilize resources  na pandemic,” amesema.

Amesema aina hiyo ya chanjo haijajulikana kuwa atazaliwa mtu wa namna gani baada ya miaka 10, kwamba kwa kawaida chanjo zote kabla ya kutumika ni lazima ziwe zimeruhusiwa na taasisi za nchini Marekani za CDC na FDA.

Hata hivyo, amesema chanjo ya corona hazikuruhusiwa na taasisi hizo  bali zimeruhusiwa na mamlaka ya dharura ambayo inasema madhara yanayotokana na chanjo hiyo ni juu ya mtumiaji mwenyewe.

Askofu Gwajima aitahadharisha Serikali kuhusu chanjo za corona

“Serikali na wizara ya afya wawe makini wanapochagua chanjo hizi  waangalie madhara ya sasa, siku zijazo na Taifa. Tatizo tulilonalo ni kudhani kila kinachotoka Ulaya kinatufaa sisi,” amesema.

Ameitaka wizara ya Afya kabla kuamua kuitumia wawe na wataalam watakaoangalia kwa makini vitu vilivyomo kwenye chanjo hiyo na matatizo watakayoyapata watu watakaozaliwa baadaye.

Amesema ni ujinga mkubwa kuruhusu majaribio ya chanjo hiyo kwa Watanzania wote kwa sababu ya haraka.