Atupwa jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka minne

Ludewa. Mahakama ya Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe imemuhukumu kifungo cha maisha jela, Simon Msanga (24), mkazi wa kijiji cha Kiwe wilayani Ludewa kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka minne.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa, Issac Ayengo alisema mshtikwa alitenda kosa hilo Mei 30, 2022 saa 10 jioni, baada ya kufika kwenye nyumba ya familia ya huyo mtoto na kumkuta akiwa nje anacheza, kisha kumchukua na kuingia naye kichakani.

Alisema wakati akiingia naye kichakani kaka wa mtoto huyo alikuwa ndani na alimwona mtuhumiwa akimchukua mdogo wake kisha akamfuata kimyakimya na kumshuhudia akimvua nguo ndipo akakimbia kwenda kumfuata mama yao ambaye alikuwa kanisani kwa wakati huo na kumjulisha tukio linaloendelea nyumbani kwao.

Aliongeza alipokaribia kufika nyumbani walikutana na mtuhumiwa ndipo kaka wa mtoto huyo alimwonesha mama yake, lakini mama huyo alikimbia kumkagua mwanae kwanza na kumkuta ameharibiwa ndipo akamfuata mtuhumiwa ambaye alikuwa katika kilabu cha pombe na kuomba msaada kwa watu wa kumkamata na kumfikisha kituo cha polisi na kisha mahakamani.

Ayengo alisema amesikiliza ushahidi wa pande zote mbili, huku ushahidi wa upande wa mashtaka ukionekana kuwa na nguvu na kuamua kutoa hukumu hiyo kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 131 (3) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2022

Naye mwendesha mashtaka wa Serikali, Angelo Marko aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo ili iwe fundisho kwake na kwa wote wenye tabia kama hizo.

Kwa upande wake, mshtakiwa kwenye utetezi wake aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwakuwa ana tatizo la kiafya la kuugua ugonjwa wa kifafa lakini mahakama ikamuamuru kutumikia kifungo hicho kwa mujibu wa sheria.