Atupwa jela miaka 30 kwa kumbaka mtoto mwenye mtindio wa ubongo

Muktasari:

  • Mahakama wilayani Siha mkoani Kilimanjaro imemhukumu mkazi wa wilaya hiyo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka msichana mwenye mtindio wa ubongo.

Siha. Mkazi wa Kijiji cha Sanya Hoyee kilichopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Ayubu Salungo (24), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka msichana wa miaka 16 mwenye mtindio wa ubongo.

Mwendesha Mashtaka, David Chisimba amesema mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elibahati Petro kuwa tukio hilo lilitokea Semptemba 20, 2023.

Amesema siku ya tukio, mshtakiwa alikuwa anafanya shughuli za ufundi, ndipo alimuona binti huyo anakwenda kuchota maji kwenye nyumba jirani na hakukuwa na mtu mwingine wakati huo.

Amesema kijana huyo alimfuata na kumshika mkono na kumuingiza chooni na kumfanyia kitendo hicho.

Chisimba amesema kumbe kulikuwa na mtu anaona kitendo hicho, ndipo alipochukua jukumu la kufunga mlango kwa nje na kupiga kelele za kuomba msaada, na wananchi walifika na kumkamata na kumpeleka kwenye vyombo vya sheria.

Amesema kitendo alichokifanya ni kinyume na kifungu namba 130 (1)(2) na 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 na kesi hiyo ilikuwa na mashahidi watano akiwamo daktari, mwathirika mwenyewe pamoja na jirani. 

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Hakimu alimpa fursa mshtakiwa kujitetea, ndipo aliomba Mahakama imwonee huruma kwa kuwa ni mra yake ya kwanza kutenda kosa hilo na kwamba ana mtoto anayemtegemea.

Hata hivyo, Mahakama imesema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama, inamhukumu kwenda jela miaka 30.

“Ni kweli vitendo vya ubakaji na ulawiti vinazidi kuongeza ndani ya wilaya yetu, ili iwe fundisho kwa wengine, unakwenda kutumikia kifungo cha miaka 30,” amesema hakimu.