Auawa baada ya kufumaniwa na mke wa mtu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamshikilia Mohamedi Lukindo (43) mkazi wa Chanika wilayani Handenia akituhumiwa kumshambulia hadi kufa Athumani Dolly (46) akidai kumfumania na mkewe nyumbani kwake usiku.


Handeni. Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamshikilia Mohamedi Lukindo (43) mkazi wa Chanika wilayani Handeni akituhumiwa kumshambulia hadi kufa Athumani Dolly (46) akidai kumfumania na mkewe nyumbani kwake usiku.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa marehemu Athumani, ameuawa usiku wa kuamkia leo Jumatatu Machi 28 baada ya kukutwa ndani na mume wa Rehema Barau majira ya usiku na kuanza kumshambulia.

Amesema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa wa mauaji kumshambulia hadi kufa kijana aliyemkuta ndani kwake na mkewe ambapo polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kujua undani wake, muhusika aliyefanya tukio hilo ameshakamatwa.

"Ni kweli kumetokea tukio la mauaji na chanzo chake ni wivu wa kimapenzi ambapo, Mohamed Lukindo amemshambulia hadi kifo Athumani Dolly baada ya kumfumania na mkewe nyumbani kwake, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na tutatoa taarifa zaidi," amesema Kamanda Jongo.

Akisimulia mkasa huo, shuhuda wa tukio hilo Asha Mwaliko amesema ilikuwa majira ya saa sita usiku, ambapo jirani yake Rehema Barua (mke wa mtuhumiwa) alikwenda kumuamsha ili amsaidie ugomvi baada ya yeye kufumaniwa na mumewe ndani kwao.

Amesema baadaye walisikia ukimya umetawala, hadi walipokuja kugundua kuwa mwanaume aliyedaiwa kufumaniwa amefariki dunia.

"Hizo vurugu zilianzia saa sita usiku, hadi kunatulia ni kama saa nane hivi, mke wa jirani alikuja kuniamsha ili nikaamue ugomvi wake na mumewe akidai amefumaniwa, ila nilishindwa kwa kuwa mimi ni mwanamke na mume wangu amesafiri," amesema Asha.

Mganga mfawidhi hospitali ya mji Handeni, Hudi Shehdad amekiri kupokea mwili wa marehemu na kueleza kuwa wanasubiri taratibu nyingine kufanyika na baadae kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.