Auwa akijaribu kupora pikipiki

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.

Muktasari:

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kuuawa kwa mtu anayedhaniwa kuwa jambazi alipojaribu kupora pikipiki akitumia silaha aina ya bastola.

Moshi. Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kuuwawa kwa mtu anayedhaniwa kuwa jambazi alipokuwa akijaribu kupora pikipiki mmoja wa madereva wa pikipiki eneo la Mabungo Himo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 27, 2022, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema, tukio hilo limetokea Oktoba 26 saa 2 usiku.

Amesema mtu huyo ambaye mpaka sasa hajatambulika majina yake anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35 alikuwa na tabia ya wizi wa pikipiki na unyanganyi wa kutumia silaha.

"Askari polisi waliokua doria walifanikiwa kufika eneo la tukio na kuwazuia wananchi wasiendelee kumshambulia jambazi huyo kwa mawe kufanikiwa kumyanganya jambazi huyo silaha pistol aina ya Brown yenye namba A.920580 ikiwa na risasi 9," amesema kamanda Maigwa.

Amefafanua kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa silaha hiyo inamilikiwa kihalali na iliibwa kutoka kutoka kwa mmiliki wake mkoani Manyara.

Ameongeza kuwa jambazi huyo alifariki dunia wakati akipelekwa hospitali kwa matibabu ambapo mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kwa utambuzi na uchunguzi zaidi unaendelea.