Aweso aivunja menejimenti ya Mwauwasa, aonya uzembe
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Uamuzi huo umefuatia ziara ya kikazi aliyoifanya waziri jijini Mwanza, ambapo amebaini uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na udhaifu wa kiutendaji.
Mwanza. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameivunja Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha utoaji huduma ya majisafi na salama jijini Mwanza.
Uamuzi huo umefuatia ziara ya kikazi aliyoifanya Waziri jijini Mwanza, ambapo amebaini uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na udhaifu wa kiutendaji.
Akizungumza na watumishi wa Mwauwasa, leo Jumanne, Juni 16, 2026, Waziri Aweso amesema licha ya mamlaka hiyo kuwa miongoni mwa taasisi bora za maji nchini, utendaji wake wa sasa hauendani na matarajio ya Serikali na wananchi.
“Kwa sasa siridhishwi na utendaji wa Mwauwasa na nyinyi wenyewe mmekiri. Asilimia kubwa ya changamoto nilizobaini kwenye ziara yangu ni za kiutendaji,” amesema Aweso.
Amesema amekuwa akitoa maelekezo mara kwa mara kwa menejimenti ya Mwauwasa kuhusu umuhimu wa uwajibikaji na kuongeza ufanisi, lakini hakuna mabadiliko aliyoyaona.
“Naivunja menejimenti ya Mwauwasa na kuanza upya. Tutatengeneza timu mpya ya watendaji kwa dhumuni la kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi wa taasisi hii muhimu,” amesema Aweso.
Waziri Aweso amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha menejimenti mpya itakayoundwa itawajibika kikamilifu katika kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Mwanza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema Wizara haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi wasiowajibika katika maeneo yote nchini.
“Wizara itaendelea kufuatilia utendaji kwa karibu. Nawasisitiza watumishi wa Mwauwasa kubadilika, kwani uwajibikaji wenu ndio utakaopunguza changamoto zinazowakabili wananchi,” amesema Mwajuma.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Buswelu wilaya ya Ilemela wameiomba Serikalia kufanya jitihada za kupatikana kwa maji kwani inakwamisha katika jitihada za kimaendeleo katika mkoa huo.
Costantin Katembo amesema:“Uhalisia wa maji kweli hali ni ngumu tunapata majia Alhamisi hadi Alhamisi ijayo, huduma zandani kuoga, choo tunashindwa. Naiomba serikali itupatie maji siku zote bila ya kuwa na mgao.”
Daudi Komanya mkazi wa Buswelu anasema:“Sisi wananchi hicho kitendo kinatuumiza sana kupata maji mara moja au tusipate kabisa katika wiki.“
Donadi Kimambo anasema:“Serikali ituangalie kwa jicho la pili tuna pata changamoto ya maji tunateseka hadi kuamua kuchimba visima.”