Aweso ataka utafiti chanzo cha maji wilayani Same
Muktasari:
- Waziri wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa maji bonde la Pangani kufanya utafiti wa chanzo cha maji katika kata ya Bendera wilayani Same kwa kuwa wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa maji kwa zaidi ya miaka 10.
Same. Waziri wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa maji bonde la Pangani kufanya utafiti wa chanzo cha maji katika kata ya Bendera wilayani Same kwa kuwa wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na ukosefu wa maji kwa zaidi ya miaka 10.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 8, 2021 katika ziara yake kata za Kihurio na Bendera zinazokabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.
"Sitakuwa kikwazo kwa wananchi wa Same na Bendera kupata maji safi ya kutosha, kero zenu nimezisikia na ndio maana Serikali imetenga Sh1.2 bilioni kutatua changamoto ya maji.”
"Niwaombe wataalamu wa bonde la pangani mshirikiane na wananchi wa eneo la Bendera mfanye tafiti ya kutafuta chanzo cha maji katika kata hii ili wananchi hawa wapate maji safi na ya kutosheleza," amesema.
Ameongeza, “watu wa bonde la Pangani mpo na tumewaanzisha mahsusi kwa ajili ya kufanya tafiti ili watueleze wapi ambapo kuna maji na kama hakuna chanzo kabisa cha maji muangalie namna ya kuchimba mabwawa na hapa mnaweza kuanzisha mradi mkubwa na wananchi hawa wakawa na mradi wao ambapo watapata maji safi na salama.”