Baba adaiwa kutumia panga kuwaunguza wanawe makalio

Baba adaiwa kutumia panga kuwaunguza wanawe makalio

Muktasari:

  • Mkazi wa Kata ya Marangu Mashariki wilayani hapa, Baltazari Mtui anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwaunguza makalio watoto wake wawili wa kiume.

Moshi. Mkazi wa Kata ya Marangu Mashariki wilayani hapa, Baltazari Mtui anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwaunguza makalio watoto wake wawili wa kiume.

Inadaiwa kuwa baba huyo aliweka panga kwenye moto kisha akawaunguza watoto hao ambao ni wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili katika Shule ya Msingi Lyasongoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale alithibitisha kutokea tukio hilo Aprili 16, mwaka huu.

Alisema wanamshikilia Mtui kwa kosa la kujeruhi na kwamba, taratibu zikikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Ni kweli tukio hili lipo na bahati nzuri mtuhumiwa amekamatwa na kesi inaandaliwa kwa ajili ya kupelekwa mahakamani,” alisema Kamanda Kakwale.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lyasongoro, Jackson Mkonyi alisema, “walichofanyiwa na baba yao inaonekana si mara ya kwanza, wameteswa kwa muda mrefu, baada ya kupigiwa simu na msamaria mwema kunieleza wanavyofanyiwa ukatili kwa kuchomwa kwenye makalio na panga lenye moto, nilikwenda hadi nyumbani kwao kuwaona, nilipowachunguza na kuwakagua kwa kweli walikuwa wameumizwa vibaya sehemu za makalioni.”

Alibainisha kuwa walifanyiwa ukatili huo Ijumaa ya Aprili 16 na walibainika Jumatatu.

“Watoto walikwenda shule Jumatatu, walivyorudi walikutana na msamaria mwema njiani, mwendo wao ulimtia shaka ikabidi awahoji, ndipo wakasema baba yao alikuwa akiwapiga na kuwafungia ndani na siku ya Ijumaa walichomwa na panga lenye moto kwenye makalio.

“Yule mama aliwashusha kaptula, alipoona yale majeraha makubwa alinipigia simu na kunieleza, nilichukua mgambo, nilipofika nyumbani kwao nilikuta wanalia, nikawauliza mmefanyaje wakasema baba yao kawachoma moto kwenye makalio,” alisema mwenyekiti huyo.

“Nililia nilipoona waliunguzwa kama nyama imechomwa, niliwapeleka hospitali wakapatiwe matibabu kwanza.”

Mkonyi alisema aliwakuta watoto hao na alama kwenye makalio zinazoonyesha kuwa ni za muda mrefu.

Jirani wa watoto hao, Anna Shao alisema walikuwa wakicheza nyumbani kwake ila tangu Aprili 16 hakuwaona.

“Nilizoea kuwaona, ila kuanzia siku hiyo sikuwaona, ikabidi nifuatilie kuna nini maana nimewazoea,” alisema Anna.

“Jumatatu wakati wanatoka shule huyu mmoja alikuwa anatembea kwa shida, ikabidi tumwangalie, tulimshusha suruali yake tulishangaa wanawake wote tuliokuwa pale. Tunaomba sheria ichukue mkondo wake,” alisema Anna.