Bashe apiga ‘stop’ fedha sekta ya kilimo kupelekwa kwenye mafunzo

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe awapa neno wadau wa maendeleo wanaotoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kwenye sekta ya kilimo

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amewataka wadau wa maendeleo wanaotoa fedha katika sekta ya kilimo kuacha kutoa fedha kwenye miradi inayohusisha mafunzo na kujenga uwezo na badala yake fedha ziwe kwenye miradi inayotatua changamoto kwenye sekta hiyo.

 Akizungumza leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wakulima, Bashe amesema kinachohitajika sasa si mafunzo bali miradi yenye tija.

“Wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo ila sehemu kubwa ya fedha hizo zinaenda kwenye kujengeana uwezo na mafunzo nasema sasa imetosha, haya mafunzo tulishapata tangu nchi inapata uhuru.

“Niwaombee wadau wa maendeleo wasitelekeze mradi wowote wa kilimo bila kupata ridhaa ya wizara na kujua fedha wanazotoa zinaenda kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta,”.

Bashe amesema ni rai ya Serikali kuona fedha za miradi katika sekta hiyo zinaenda kujenga miundombinu wezeshi ya kilimo.