Bashe atoa miezi mitatu kuhakiki mikataba Kilimanjaro

Wednesday October 06 2021
bashepic
By Fina Lyimo

Moshi. Naibu waziri wa kilimo, Hussen Bashe ametoa miezi mitatu kwa kamati kuhakiki mikataba ya mashamba ya ushirika Mkoa wa Kilimanjaro na kuweka makubaliano ya pamoja na wawekezaji ili kumaliza migogoro.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 6, 2021 mjini hapa, Naibu Waziri Bashe amesema aliunda kamati ambayo imeshapitia mashamba 20 ya Wilaya ya Hai na Siha na kuja na uamuzi wa pamoja kati mwekezaji na viongozi wa ushirika.

Amesema lengo la kamati hiyo ni kuondoa mikataba mibovu iliyokuwa imeingiwa kati ya wawekezaji na wanaushirika pamoja kusimamia makubaliano ya ushirika na wewekezaji.

"Mwekezaji anakodisha shamba kwa vyama vya msingi kwa muda mrefu kwa makubaliano ya kulima kahawa lakini wanakiuka mikataba na kuanza kufanya uwekezaji wa kitu kingine. Mashamba kama hayo yote yarejeshwa kwenye vyama vya msingi, ili kuwekwe mikataba mipya ambayo itanufaisha wana ushirika"

Kwa upande wake Kaimu Mrajisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jackline Senzaghe amesema kamati hiyo tayari imepitia mashamba 20 ya wilaya ya Hai na Siha na kuwekwa kwa makubaliano kati ya vyama vya msingi vya ushirika.

Amesema wilaya hizo zina mashamba 40 na kwamba mashamba 20 yaliyobaki ndani ya miezi mitatu watakuwa wamepitia pamoja na kurekebisha mikataba mibovu iliyoingiwa hapo awali.

Advertisement


Naye Mkurugenzi wa Shamba la Tudeley Estate, Jensen Natai, amesema aliwekeza katika samba hilo lenye hekari 2050 kwa zaidi ya miaka 24 na kwamba kwa miaka miwili iliyopita ameshindwa kulipa dola za kimarekani 130 kwa hekari.

Amesema kutokana na hali hiyo yuko tayari kuvunja mkataba ili aweze kuomba hekari 250 ambazo anaweza kuwekeza.Advertisement