Bashungwa, Aweso wamwakilisha Rais Samia kupokea kero

Friday May 20 2022
bashungwa pc
By Robert Kakwesi

Tabora. Mawaziri wawili wa sekta za Maji na Tamisemi wamekutana na makundi maalumu yanayowakilisha na kuendesha shughuli za kiuchumi zinazotegemewa na wananchi mkoani hapa.

Mawaziri hao ni Innocent Bashungwa wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Jumaa Aweso wa Maji ambao walikutana juzi Mei 18 na makundi hayo katika mkutano maalumu uliopewa jina la 'Sema na Mama' baada ya kuagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yuko mkoani Tabora kwa ziara ya siku tatu.

Makundi hayo yanajumuisha wenye ulemavu, waendesha bodaboda na bajaji, wajasiriamali na wamachinga wanaondesha shughuli zao mkoani hapa, mafundi ujenzi na wafugaji ambao walitoa maoni na changamoto kuhusu vikwazo vinavyowakwamisha kusonga mbele katika kujikwamua na umaskini.

Akizungumza mbele ya mawaziri hao, Donatus Rupoli mwenye mlemavu wa macho, alitaka watoto wa wenye chngamoto hiyo, kupewa kipaumbele katika ajira kama inavyofanyika sasa kwa wenye ulemavu.

Akitoa sababu zake, Rupoli amesema wapo wenye ulemavu ambao kutokana na umri mkubwa hawawezi kuajiriwa na badala yake wapewe fursa hiyo watoto wao.

Pia, ametaka wenye ulemavu waondolewe kodi kutokana na hali zao ambazo zinawafanya watumie fedha nyingi zaidi kuliko wale wasio na ulemavu na kwamba kuondolewa kodi kutawapa ahueni na kupiga hatua katika biashara zao.

Advertisement

Mratibu wa wajasiriamali Ashura Mwazembe ametaka elimu itolewe kwa wanaosindika vyakula na wafugaji wa nyuki, walitaka elimu na mafunzo zaidi pamoja na kuitaka Serikali kujenga kiwanda cha kutengeneza vifungashio.

“Bidhaa zao zina bei mdogo lakini zinaongezeka kutokana na vifungashio ambavyo ni changamoto kwao.Changamoto nyingine ni kukosa vigezo na kushindwa kufanya bidhaa zao zipate masoko ndani na nje kwa kukosa alama ya ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mwenyekiti wa wamaachinga mkoa wa Tabora, Zubery Omary aliomba kuboreshwa kwa miundombinu katika maeneo waliyotengewa ili mazingira ya kufanyia kazi yawe mazuri zaidi.

bashungwa pcc

Kabla ya kujibu changamoto hizo, mawaziri hao walielezea sera, mikakati na programu za Serikali zinazolenga kusimamia malengo ya kiuchumi ili kuwakwamua Watanzania.

Akijibu changamoto hizo, Bashungwa ameeleza kukubali kwamba wenye ulemavu wasio walimu nao kuwa na umuhimu wa kupata mafunzo ya kompyuta na watoto wa wazazi wenye ulemavu kifikiriwa kupewa kipaumbele katika ajira ambayo ameyachukua kuyafanyia kazi.

Kuhusu walemavu kusamehewa kodi, Bashungwa alieleza dhamira ya Serikali kuwasaidia wenye ulemavu lakini changamoto ni wao kutumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, jambo ambalo linaleta shida. Alisema serikali itaangalia namna ya kuwasaidia.

Bashungwa akizungumza pia kuhusu wajasiriamali kukosa nembo ya ubora na masoko, akisema atawaagiza viongozi wa TBS na Sido (Shirika la Viwanda Vidogo vidogo) kwenda Tabora kuonana na mkuu wa mkoa huo ili kuratibu mchakato huo.

Bashungwa ameeleza pia upande wa kuboresha maeneo ya machinga, akisema wanataka kujenga majengo kwa ajili ya machinga ambayo yatafanana na lile la Dodoma na tayari Rais Samia ameshatoa Sh5 bilioni za kuanzia na wanatafuta fedha zingine kwa ajili ya utekelezaji.

Kuhusu majeruhi wa ajali za bodaboda, aliagiza wawe wanatibiwa wakati taratibu zingine katika mfumo zikiendelea na sio kusubiri na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kusimamia.

Naye Aweso, amesema changamoto kubwa kwa vijana na makundi maalum ni mitaji na kuwaahidi Serikali itashughulikia huku akiwatoa hofu kwa wao viongozi vijana wamepata dhamana kubwa ndani ya Taifa hivyo, hawatawaangusha katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Tutawatetea na kuwasemea maana maisha mnayoishi tunayafahamu, anayelala na mgonjwa ndiye anajua mihemko ya mgonjwa.Rais Samia alikabidhiwa nchi ikiwa katika kipindi kigumu lakini amekuwa imara na kila changamoto ameweza kuitafutia ufumbuzi,” amesema Aweso.

Advertisement