Bawacha: Muulizeni Ndugai kina Mdee ni wabunge wa chama gani
Muktasari:
- Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limetaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kuulizwa sababu za wanawake 19 waliofukuzwa uanachama wa chama hicho kuendelea kuwa wabunge wa viti maalum.
Dodoma. Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limetaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kuulizwa sababu za wanawake 19 waliofukuzwa uanachama wa chama hicho kuendelea kuwa wabunge wa viti maalum.
Pia limeviomba vyombo vya habari vikiripoti habari kuhusu wanawake hao wakiongozwa na Halima Mdee, kutoandika kuwa ni wanachama wa Chadema kwa kuwa wameshafukuzwa.
Novemba 27, 2020 mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza Mdee na wenzake 18 kuvuliwa uanachama wa chama hicho kwa sababu wamekiuka katiba na kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila chama hicho kuwapitisha.
Waliovuliwa uanachama ni Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Mbowe alitaja hatua nyingine tatu ambazo kamati kuu imezichukua ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa miongoni mwao waliokuwa viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na lile la wanawake (Bawacha) na kuagiza mchakato wa kujaza nafasi zao uanze mara moja.
Akizungumza leo Jumatano Aprili 21, 2021 kwa niaba ya makamu mwenyekiti wa baraza hilo, mweka hazina wa Bawacha, Catherine Ruge aliwaomba wanahabari kumuuliza Ndugai wabunge hao wanatoka chama gani cha siasa.
“Hivi hamuwezi kujiuliza kwamba hata hapo walipo wanawakilisha halmashauri zipi, maana mbunge wa viti maalumu lazima uwe na halmashauri lakini wao wapo tu na hakuna mahali popote wanapowajibika zaidi ya maslahi yao,” amesema Ruge.
Kuhusu rufaa waliyokata amesema ni haki yao na kuongeza kuwa walipaswa kuwa wamejiondoa lakini kutofanya hivyo ni kukaidi maagizo ya chama ambalo ni kosa jingine.