Benki ya Absa yadhamiria kuondoa pengo la teknolojia kijinsia
Dar es Salaam. Katika jitihada za kupunguza pengo la kijinsia katika sekta ya teknolojia nchini, Benki ya Absa Tanzania imeendeleza dhamira yake ya kuwawezesha wanawake kupitia shindano la ubunifu la GirlCode Hackathon 2025, lililofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Tukio hilo, lililodumu kwa saa 36 mfululizo, liliwakutanisha wasichana wabunifu, watengeneza programu, na wajasiriamali vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, chini ya uratibu wa Women in Tech Centre na Girl Code Africa. Lengo kuu lilikuwa kuwapa jukwaa la kubuni suluhisho za kidijitali zinazolenga kukabiliana na changamoto katika nyanja za Teknolojia ya Fedha (Fintech), Akili Unde (AI), na Usalama wa Mtandao (Cybersecurity).
Akizungumza leo Oktoba 14, 2025 alipokuwa akifunga hafla hiyo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya Absa Tanzania, Patrick Foya amesema kuwa GirlCode Hackathon ni zaidi ya shindano la teknolojia, kwani limekuwa jukwaa la kujifunza, kushirikiana na kujenga kizazi kipya cha wanawake viongozi katika sekta ya teknolojia.
“Wanawake wanapopewa nafasi, hawashiriki tu bali wanaongoza. Kizazi kijacho cha viongozi wa teknolojia tayari kipo, na kina nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko katika uchumi wa kidijitali,” amesema Foya.
Ameongeza kuwa washiriki wa mwaka huu wameonyesha uwezo mkubwa wa kufikiri kwa undani na kutatua changamoto kwa njia bunifu, hasa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitawaliwa na wanaume.
“Suluhisho mlizotoa si tu za kuvutia kiteknolojia, bali zinagusa maisha halisi ya Watanzania. Mmeonyesha kuwa ubunifu hauna jinsia, na mustakabali wa teknolojia nchini uko mikononi mwa wanawake kama ninyi,” amesisitiza.
Foya amefafanua kuwa Benki ya Absa imejikita katika kukuza vipaji vya wanawake vijana kupitia mafunzo, ushauri, na programu za kuwajengea uwezo, sambamba na kauli mbiu ya benki hiyo inayosema ‘Kuimarisha Kesho ya Afrika Pamoja, Kisa Kimoja kwa Wakati’.
“Matukio kama haya hayahusu tu uandishi wa programu, bali ni kuhusu kujenga njia endelevu. Tunatambua vipaji, tunalea uwezo, na kufungua milango ya fursa. Tunataka kuhakikisha washiriki hawa wanapata nafasi za kujifunza zaidi, kupata ajira, na kuwa sehemu ya suluhisho za kiteknolojia za baadaye,” amesema.
Mkurugenzi wa Teknolojia wa benki hiyo, Emanuel Mwinuka amesema kuwa mpango wa GirlCode Hackathon ni sehemu ya juhudi za kimkakati za benki hiyo katika kupunguza pengo la kijinsia katika taaluma za kompyuta na teknolojia nchini, pengo ambalo bado ni kubwa katika maeneo mengi ya kazi.
“Changamoto ya usawa wa kijinsia katika sekta ya teknolojia haipo tu katika benki, bali inajitokeza katika tasnia nzima. Ndiyo maana tumeamua kuhamasisha wanawake vijana kutoka vyuoni na sehemu za kazi kujitokeza, kutumia teknolojia kutatua matatizo, na kujenga mustakabali unaojumuisha wote,” amesema Mwinuka.
Amesema kupitia mashindano hayo, washiriki wamepata nafasi ya kujifunza teknolojia za kisasa, ikiwemo akili bandia na mifumo ya usalama wa kimtandao, ambapo programu kama hizo zinasaidia kuandaa kizazi cha wanawake watakaoweza kushindana kimataifa.
“Tukio la leo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Tumepata washindi watatu, na mshindi wa kwanza atawakilisha Tanzania kushindana na washindi kutoka mataifa mengine kupitia suluhisho walizounda. Tunatarajia kuona wanawake hawa wakiendelea kung’ara katika sekta ya teknolojia ndani na nje ya nchi,” amesema.
Mmoja wa washiriki wa GirlCode Hackathon 2025, Mariam Saidi Mohammed, ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza programu, amesema tukio hilo limempa uzoefu mkubwa na kuimarisha kujiamini kwake katika kuunda suluhisho za kidijitali.
“Nimejifunza kuwa teknolojia si ya wanaume pekee. Kama wanawake tutatumia ubunifu wetu vizuri, tunaweza kutatua matatizo mengi ya jamii. Ninawahamasisha wanawake wengine wajitokeze, wasiwe na hofu,” amesema Mariam.