Biashara zaanza kurejea Hanang'

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hadi jana Desemba 5, 2023 watu 65 walipoteza maisha huku 116 wakijeruhiwa na wengine wakipoteza makazi yao ambapo yamefunikwa na tope, mawe makubwa na magogo ya miti.

Hanang. Baadhi ya wafanyabiashara katika mji wa Katesh, wilayani Hanang wameonekana wakifanya usafi katika maeneo yao ya biashara kwa kutoa matope yaliyosababishwa na maporomoko kutoka mlima Hanang.

Leo Jumatano Desemba 6, 2023 ikiwa ni siku ya nne tangu kutokea kwa maafa hayo, Mwananchi Digital imeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiendelea kusafisha maeneo yao ya biashara.

Aidha idadi ya maduka yaliyofunguliwa kwa ajili ya kuendelea na  biashara yameongezeka, ikiwa  tofauti na hali iliyokuwepo juzi na jana ambapo mengi yalikuwa yamefungwa.

New Content Item (1)


Miundombinu  ya barabara inazidi kufunguka ambapo wananchi kwa kushirikiana na vikosi vya uokoaji wanaendelea kutoa tope lililokuwa limejaa barabarani na kwenye mitaro ya maji iliyopo pembezoni mwa barabara kuu, huku barabara za ndani zikiendelea kusafishwa pia.

Usiku wa kuamkia leo mvua ilinyesha kwa saa kadhaa kabla haijakatika ambapo shughuli za uokoaji waathirika wa maporomoko hayo zikiongozwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama likiendelea.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hadi jana Desemba 5, 2023 watu 65 walipoteza maisha, 116 wakijeruhiwa na wengine wakipoteza makazi yao ambapo yamefunikwa na tope, mawe makubwa na magogo ya miti.