Bilioni 6 zatengwa ukarabati wa barabara Temeke

Muktasari:

  • Kiasi cha fedha zaidi ya shilingi bilioni sita kimetengwa kwa ajili ya kutatua changamoto za barabara ndani ya manispaa ya Temeke katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24

Dar es Salaam. Kiasi cha fedha zaidi ya shilingi bilioni sita kimetengwa kwa ajili ya kutatua changamoto za barabara ndani ya manispaa ya Temeke katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini(TARURA) wilaya ya Temeke Injinia Paul Mhere  katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara kwa mwaka 2022/23 na mpango wa mapendekezo ya bajeti ya 2023/24 kilichofanyika ukumbi wa Iddi Nyundo.

Akizungumza na waandishi wa  habari baada ya kikao cha baraza la madiwani na wataalamu wa manispaa ya Temeke ,Mhere amesema kiasi hicho kimetengwa ili kuondoa changamoto za ubovu wa barabara hizo ambazo zitajengwa kwa viwango tofauti ikiwemo changarawe, zege na nyingine kwa kiwango cha lami.

"Fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2023/24 kutoka katika mapato ya ndani, mfuTarura inatarajia kufanya matengenezo ya barabara zenye jumla ya  urefu wa Km 262.68 kutoka katika kata zote 23 za wilaya hii"

Amesema baada ya utekelezaji wa mpango huu hali ya barabara itaimarika na kuboreshwa kutoka 87.64% ya upitikaji hadi 91.66%.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika alisema anaamini kupitia mpango huo wa Tarura kwa mwaka wa fedha 2023/24 utakwenda kuleta mabadiliko kupitia maboresho ya miundombinu ya barabara.

Nae Diwani wa Viti Maalum Chikole Abdallah amesema amefurahishwa na mpango huo kwani hata baadhi ya barabara zilizokuwa korofi katika eneo lake ikiwemo ile inayojulikana kama Jerusalem.